NEWS

Saturday, 11 April 2026

Mara Online yatunukiwa Cheti cha Shukrani kwa mchango uliofanikisha Siku ya Tuzo za Walimu Tarime Mji



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kulia), akimkabidhi mwakilishi wa Mara Online, Fedrica Philace, Cheti cha Shukrani kilichotolewa na Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Halmashauri ya Mji wa Tarime imeitunuku Mara Online Cheti cha Shukrani, ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wake katika kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Tuzo za Walimu kwenye halmashauri hiyo.

Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, alikabidhi cheti hicho kwa mwakilishi wa Mara Online, Fedrica Philace, wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika Aprili 10, 2026 mjini Tarime.

“Cheti hiki kimetolewa kwa Mara Online Limited kwa kutambua na kuthamini moyo wako wa kujitolea, ukarimu na mchango wako wa hali na mali uliowezesha kwa kiasi kikubwa kufanikisha shughuli ya Siku ya Tuzo.

“Ushirikiano wako ni nguzo ya maendeleo yetu. Tunatoa shukrani za dhati na tunakutakia mafanikio mema,” inaeleza sehemu ya maneno yaliyopo kwenye cheti hicho cha shukrani.

Mbali na DC Gowele, hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wengine wa serikali, akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo, walimu na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Tuzo za Walimu yalilenga kutambua na kuwatunuku walimu waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za ufundishaji na malezi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ubora na uwajibikaji katika sekta ya elimu ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ya Siku ya Tuzo za Walimu inasema: “Kuthamini Walimu ni Msingi wa Elimu Bora na Taifa Imara”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages