
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (katikati), akikabidhi mchango katika harambee ujenzi wa ofisi ya Kanisa la SDA Jimbo jipya la North Mara Field, leo Aprili 11, 2026.
Mara Online News
Tarime
---------------
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, ameongoza harambee iliyokusanya shilingi milioni 641 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Jimbo jipya la North Mara Field.
Waziri Nyansaho ambaye amemwakilisha Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba na ujumbe wake, wamechangia shilingi miloni 82 katika changisho hilo ambalo limefanyika leo Aprili 11, 2026 katika Kanisa la SDA la MUMAS (Kibumaye), nje kidogo ya mji wa Tarime.
Washiriki kutoka makanisa yote ya SDA ya jimbo hilo na wadau wengine wamechangia shilingi milioni 559.
“Inaonekana nimekuja na mibaraka, kwa jinsi matoleo ya leo yalivyokwenda, ujenzi wa jengo la ofisi ya SDA North Mara Field utakamilika na jengo litasimama,” Waziri Nyansaho amesema katika sehemu ya hotuba yake fupi.

Waziri Nyansaho akizungumza katika harambee hiyo
Waziri Nyansaho amembatana na viongozi mbalimbali, wakiwemo mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Mkoa wa Mara, Christopher Mwita Gachuma, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.
Askofu wa Kanisa la SDA Jimbo la North Mara Field, Dkt. Benjamin Ngalama Biha, amemshukuu Waziri Nyansaho na viongozi wengine kwa kushiriki katika changizo hilo.
Ujenzi wa jengo la ofisi ya SDA Jimbo la North Mara Field ambalo litakutwa la ghorofa mbili, unatarajiwa kufanyika kwa miaka miwili kuanzia mwaka huu, kwa mujibu wa taarifa ilisomwa kwa Waziri Nyansaho.
Aidha, ujenzi huo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.5, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Waziri Nyansaho akivishwa skafu mara baada ya kuwasili katika Kanisa la SDA Kibumaye kuongoza harambee hiyo. (Picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment