NEWS

Monday, 13 April 2026

Namba Tatu sasa akataa kuitwa mstaafu



Samwel Kiboye "Namba Tatu" akizungumza kwenye harambee ya ujenzi wa ofisi za Kanisa la SDA Jimbo la North Mara Field, mjini Tarime juzi.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
--------------

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maarufu kama Namba Tatu, ametangaza rasmi kukataa kuitwa mstaafu.

“Mimi naitwa Namba Tatu, nisiitwe mstaafu, tusubiri yajao mbeleni,” Namba Tatu alisema kwa msisitizo mjini Tarime juzi.

Ingawa Namba Tatu hakufafanua kauli yake hiyo, wadadisi wa masuala ya siasa za Mara wameitafsiri kama ujumbe wa kimkakati wa kupima upepo wa kisiasa kabla ya uchaguzi wa ndani ya CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Wengi wanaona kauli hiyo ya Namba Tatu ina dalili ya kuamsha ari ya wafuasi wake ili hatimaye aweze kurejea katika ulingo wa siasa za ushindani ndani ya chama hicho tawala.

Namba Tatu anatajwa kuwa miongoni mwa makada wenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM Mara, akiwa na historia ya uongozi iliyoanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa.

Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Tarime, Mwenezi na Mwenyekiti wa Wilaya ya Rorya kwa nyakati tofauti, kabla ya kushika wadhifa wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara kuanzia mwaka 2017 hadi 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages