NEWS

Monday, 13 April 2026

Ujenzi ofisi za SDA North Mara Field kugharimu shilingi bilioni 3.5



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (aliyevaa skafu), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (wa pili kushoto), MNEC Christopher Gachuma (kushoto) na Askofu wa Kanisa la SDA Jimbo la North Mara Field, Benjamin Ngalama Biha (kushoto kwa Waziri), wakiwa kwenye harambee ya ujenzi wa ofisi za jimbo hilo wilayani Tarime juzi.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
---------------

Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) limepanga kutumia shilingi bilioni 3.5 kugharimia ujenzi wa ofisi za makao makuu ya jimbo lake jipya la North Mara Field.

Ofisi hizo zitajengwa katika eneo la Kibumaye, nje kidogo ya mji wa Tarime, mkoani Mara ili kuimarisha huduma za kiroho na kiutawala kwa waumini wa SDA katika ukanda huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi hizo juzi, maandalizi ya awali tayari yameanza, huku jengo husika likitarajiwa kuwa la ghorofa mbili.

“Jengo litakuwa la ghorofa mbili, ambalo pia litakuwa na kumbi za ibada na mikutano… gharama zote za ujenzi zitakuwa shilingi bilioni 3.5,” ilisema sehemu ya taarifa ya kanisa hilo.

Mwonekano wa jengo la ofisi za Kanisa la SDA Jimbo la North Mara Field litakapokamilika

Taarifa hiyo ya ujenzi wa ofisi hizo za SDA North Mara Field ilisomwa mbele ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika harambee hiyo.

Kiasi cha shilingi milioni 641 kilikusanywa katika harambee hiyo - fedha ambazo zitatumika kukimbiza ujenzi huo.

“Inaonekana nimekuja na mibaraka kwa jinsi matoleo ya leo yalivyokwenda, ujenzi wa jengo la ofisi ya SDA North Mara Field utakamilika na jengo litasimama,” Waziri Nyansaho alisema katika sehemu ya hotuba yake fupi, akionesha kuguswa na mwitikio wa washiriki.

Waziri Nyansaho (katikati) akipokewa na wenyeji wake alipowasili kumwakilisha Waziri Mkuu Mwigulu katika harambee hiyo.

Waziri Nyansaho aliambatana na viongozi wengine mbalimbali, wakiwemo mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Mkoa wa Mara, Christopher Mwita Gachuma, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.

Kanali Mtambi aliipongeza SDA kwa maono yake makubwa ya maendeleo, akibainisha kuwa ujenzi wa ofisi hizo utachangia kupendezesha mandhari ya Tarime na kuinua hadhi ya mkoa wa Mara.

“Hongereni sana, jengo hili litapendezesha wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara,” alisema Kanali Mtambi.

Naye Askofu wa SDA Jimbo la North Mara Field, Dkt. Benjamini Ngalama Biha, alitoa shukrani za dhati kwa Waziri Nyansaho na viongozi wengine, wageni waalikwa na waumini wote walioshiriki kwa hali na mali kuhakikisha changizo hilo linafanikiwa.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages