
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelezea athari ya vita ya Marekani na Iran kwa dunia, ikiwemo Tanzania, hususan katika kupanda kwa bei ya mafuta na upungufu wa mafuta.
Aidha, Rais Samia amesema kutangazwa kusitishwa kwa vita hiyo na kufunguliwa kwa mlango bahari wa Hormuz ni jambo la faraja.
"Hii inatupa matumaini makubwa sana kama serikali na ile kuruhusu tu meli za awali za Ufaransa,za Japan... kidogo nimeona bei ya mafuta imeshuka kidogo, sasa hii inatupa matumaini,” Rais Samia alisema Ikulu - Chamwino, jijini Dodoma jana katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.
Lakini hata hivyo, Rais Samia aliahidi kupunguza matumizi makubwa ya mafuta serikalini kwa kuanza na ofisi yake.
"Ndani ya serikali tuna matumizi makubwa ya mafuta, magari ni mengi, safari zetu ni nyingi niwaombe sana tuanze kupunguza matumizi ya mafuta, kwa kuanza na ofisini kwangu ninapotembea kuanzia sasa wote nitawaingiza kwenye kibasi,” alisema.
Kiongozi huyo wa nchi alisema upandaji wa bei ya mafuta umekuwa ukienda sambamba na kupanda kwa bei za bidhaa, hivyo akawaomba wananchi kuwa watulivu.
No comments:
Post a Comment