Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (wa tatu kulia mbele), katika picha ya pamoja na mgeni wake, miongoni mwa viongozi wengine walipokutana makao makuu ya wizara hiyo, jijini Dodoma jana.Dodoma
--------------
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, jana Aprili 9, 2026 alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo, Guy Kabombo Muadiamvita, aliyefanya ziara ya kikazi nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo ya kikazi baina ya viongozi hao wawili yaliyofanyika katika makao makuu ya Wizara ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo jijini Dodoma, yalilenga kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria kati ya Tanzania na Congo katika diplomasia ya ulinzi.
Katika kikao hicho, Waziri Nyansaho alimhakikishia Naibu Waziri Mkuu huyo wa Congo, utayari wa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushirikiana na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali za ulinzi, hususan katika ubadilishanaji wa wataalamu, mafunzo pamoja na kupambana na changamoto za kiusalama kama vile uhalifu wa mtandaoni na vita dhidi ya ugaidi.
Waziri Nyansaho alimueleza Naibu Waziri Mkuu Kabombo kuwa ziara yake Tanzania ni ushahidi wa uhusiano thabiti uliopo kati ya nchi hizo, huku ikionesha umuhimu katika kuendelea kudumisha na kuimarisha maelewano, ushirikiano na urafiki.
Aliongeza kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na majadiliano ya wazi yenye nia ya kujenga na kuweka misingi na ushirikiano madhubuti baina ya nchi hizo mbili.
"Nina imani kuwa kupitia ushirikiano na uhusiano wetu sio tu tutakabiliana na changamoto zinazotukabili kwa pamoja, bali pia tutanufaika na fursa zilizopo mbele yetu," alisema Waziri Nyansaho.
Waziri Nyansaho alimueleza Mgeni wake huyo kuwa serikali za Tanzania na Congo zina nafasi na fursa kubwa ya kunufaika na ushirikiano wa kibiashara na uchumi, hususan katika usafirishaji wa mizigo kuputia Bandari ya Dar-es-salaam na njia nyinginezo za kiuchumi, hivyo kuboresha ustawi na maendeleo ya wananchi wa nchi hizo.
No comments:
Post a Comment