
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (kushoto), akiteta jambo na Balozi wa Dola ya Qatar nchini Tanzania, Fahad Rashid AL-Muraikhi, jijini Dodoma jana.
Dodoma
-----------------
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, jana Aprili 8, 2026 alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Dola ya Qatar nchini Tanzania, Fahad Rashid AL-Muraikhi, jijini Dodoma
Balozi Fahad alimueleza Waziri Nyansaho utayari wa Dola ya Qatar kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali yanayohusiana na Wizara ya Ulinzi na Nchi kwa ujumla.
Alisema Tanzania na Dola ya Qatar zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu ambao umekuwa chachu ya maendeleo baina ya nchi hizo.
Uhusiano huo umekuwa ukiongozwa na viongozi wakuu wa nchi ya Tanzania na Dola ya Qatari, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara ya kikazi nchini Qatar mwaka 2023.
Ziara ya Rais Samia nchini Dola ya Qatar ni kielelezo cha utayari wa Tanzania kushirikiana na taifa hilo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, utamaduni, ulinzi na kijamii.
Naye Waziri Nyansaho alimshukuru Balozi Fahad kwa kufika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa kwa ajili ya kuendeleza uhusiano wa kindugu na muda mrefu baina ya Tanzania na Qatar.
Waziri Nyansaho alimhakikishia Balozi Fahad kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Aidha, Waziri Nyansaho alimueleza Balozi Fahad utayari wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kushirikiana na nchi ya Qatar katika masuala ya ushirikiano wa kijeshi, mafunzo na kubadilishana utalaamu pamoja na kukabiliana na changamoto za kiusalama za ugaidi na uhalifu wa mtandaoni.
Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa waliokuwa na Waziri wa Ulinzi na JKT katika mazungumzo hayo ni pamoja na Kaimu Kamishna wa Utafiti na Maendeleo Jeshini, Brigedia Jenerali Josephy Kapumbe na Mkurugenzi wa Huduma ya Mipango wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Brigedia Jenerali Gerald Omary.
No comments:
Post a Comment