
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, akizungumza katika misa ya Jumapili ya Pasaka kwenye Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Mara, mjini Musoma jana Aprili 5, 2026.
Musoma
---------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, jana Aprili 5, 2026 alishiriki misa ya Jumapili ya Pasaka katika Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Mara na kuwataka viongozi wa dini na waumini wa dini mbalimbali kuliombea taifa ili nchi iendelee kuwa na umoja, amani wa mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza katika misa hiyo, RC Mtambi aliwataka wananchi wa mkoa wa Mara kutanguliza maslahi ya taifa kwanza kabla ya maslahi yoyote binafsi yanayojitokeza kwa misingi ya itikadi za kisiasa, dini na mitazamo ya kijamii pamoja na kuendelea kuiombea Tanzania na viongozi wake.
“Ninawaomba ndugu zangu tutangulize maslahi ya taifa letu kwanza, tuilinde na tuitumikie nchi yetu kwa weledi,” alisema RC Mtambi na kuongeza kuwa Watanzania hatuna taifa lingine ambalo litakuwa la kwetu tusiposhikamana na kulienzi taifa hili.
Aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa na kuliongoza katika mapambano ya mmomonyoko wa maadili katika jamii ili kujenga kizazi chenye maadili mema na kinachopinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na kukemea mila potofu katika jamiii.
Pia, RC huyo liwataka wananchi wa mkoa wa Mara kusherekea Sikukuu ya Pasaka kwa kiasi na kwa uangalifu ili kuepuka majanga yanayoweza kutokea na watumiaji wa barabara na waendesha vyombo vya moto kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani ili kujilinda na ajali.

RC Mtambi (katikati) akishiriki kuimba pamoja na viongozi na waumini katika misa hiyo
Aidha, RC Mtambi aliwataka vijana wa Tanzania kutumika kwa maslahi mapana ya taifa kwa kusaidia kueneza ujumbe muhimu wa kusambaza upendo, matumaini, amani na mshikamano kwa Watanzania wote bila kujali tofauti zao.
Vilevile, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati huu wa mvua na kuwataka wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama, kuchukua tahadhari wakati wa kuvuka mito na madaraja yaliyojaa maji ili kunusuru maisha yao, na wanaojihusisha na uchimbaji wa madini kuchukua tahadhari.
Alimwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara kuendelea kufanya ukaguzi wa migodi ya madini na kutoa ushauri kuhusiana na hali ya mgodi husika, hususan wakati huu ambapo mvua zinaendelea kunyesha nchini.
RC Mtambi alitumia fursa hiyo pia kufikisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizozitoa katika kusherekea Sikukuu ya Pasaka kwa wananchi wa mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Mara, Dkt. George Meshack Okoth, aliwataka waumini wa kanisa hilo kuzikabili changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao na kuacha kulaumu watu wengine wanaposhindwa kuzitatua changamoto hizo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.

Askofu Okoth akihubiri katika misa hiyo ya Jumapili ya Pasaka
“Watanzania tunapenda sana kulaumu, hata kwa mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu tukiamua kuyafanyia kazi, tunawalaumu wazazi, viongozi wa dini, viongozi wa serikali na tuna manung’uniko mengi kwa mambo ambayo tunatakiwa kuyatatua sisi wenyewe,” Askofu Okoth alisema katika sehemu ya mahubiri yake.
Aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwa na mipango katika maisha yao na kutafuta njia sahihi ya kufanikisha mipango hiyo na kuacha kulaumu watu wengine kama mipango hiyo haijafanikiwa katika maisha, bali wawe na subira na wamtegemee Mungu kwa ujasiri wakiamini kuwa watashinda.
Askofu Okoth alitoa mfano wa wanawake waliotajwa kwenye Biblia kuwa walioamka asubuhi kwenda kumtembelea Yesu kaburini huku wakijua kulikuwa na vikwazo vingi kwao lakini walienda kwa ujasiri kumtembelea wakiwa wamenunua manukato na mafuta ili kumsitiri Yesu kaburini.
No comments:
Post a Comment