
Simba
Na Mwandishi Wetu
Serengeti
---------------
Watu wawili wameripotiwa kujeruhiwa kwa kushambuliwa na simba katika kata ya Nagusi, wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.
Kwa mujibu wa Diwani wa kata hiyo, Andrea Mapinduzi, watu hao walishambuliwa siku na nyakati tofauti hivi karibuni, wakati wakichunga mifugo katika kitongoji cha Mbugani.
Mapinduzi aliwataja majeruhi hao kuwa ni Kura Mkurya na Kamanda Goshoo, wote wakazi wa kitongoji hicho.
“Kamanda amepata nafuu lakini Kura bado anauguza majeraha,” alisema diwani huyo.
Alieleza kwamba licha ya mamlaka husika kujizatiti kudhibiti wanyamapori wakali, simba bado wameendelea kuwa tishio kubwa kwa maisha ya wananchi wa Nagusi.
Baada ya kupata taarifa za kujeruhiwa kwa watu hao, askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Grumeti walikwenda kutega na kufanikiwa kumnasa simba mmoja.
Matukio ya simba kuvamia vijiji katika kata hiyo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na kusababisha madhara kwa binadamu na mifugo.
Hivyo, Diwani Mapinduzi aliendelea kuiomba serikali kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha kero hiyo.
“Sisi viongozi wa kata na vijiji tunaendelea kuhimiza wananchi kuchukua tahadhari, ikiwemo kutembea kwa makundi na kuepuka kupeleka mifugo kwenye maeneo yenye vichaka vikubwa,” alisisitiza.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment