
Maafisa wa TRA Mkoa wa Mara wakijitambulisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, kabla ya kwenda kuelimisha kuhusu masuala ya forodha jana.
Tarime
--------------
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imeanza kutoa elimu kwa wananchi wa wilayani Tarime kuhusu mambo ya forodha, hususan uingizaji na uondoaji bidhaa nchini.
Kabla ya kwenda kuanza utoaji wa elimu hiyo, maafisa hao wa TRA walikwenda kujitambulisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ambaye aliwapongeza kwa jitihada hizo za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya biashara na ulipaji wa kodi.
Meja Gowele alisema wafanyabiashara wanaoingiza na kutoa bidhaa nchini wana nafasi kubwa ya kuchangia mapato ya serikali iwapo watazingatia taratibu na sheria zilizowekwa kwa maendeleo ya taifa.
“Nawashukuru kwa jambo hili jema la kutoa elimu kwa wananchi wetu, hasa kwa wafanyabiashara wanaoingiza na kutoa bidhaa nchini. Kama kila mwananchi atazingatia, naamini tutaongeza mapato makubwa kwa ajili ya mambo ya msingi ya nchi yetu,” alisema.
Elimu hiyo ambayo inagusa taratibu na sheria za forodha, ilianza kutolewa jana Aprili 20, 2026 kwa wananchi wanaoishi katika mji wa Sirari uliopo mpakani na nchi ya Kenya.
Afisa Elimu na Mawasiliano kwa Umma wa TRA, Ruekaza Rwagoshora, alionya kuwa kupitisha mzigo nje ya kituo cha forodha kunalinyima taifa mapato yake na nchi inakosa taarifa muhimu kuhusu jinsi biashara inavyofanyika.
Naye Afisa wa TRA wa Kitengo cha Wateja, Emmanuel Grayson Muchunguzi, alisema serikali imeanza kuondoa ushuru kwa pembejeo zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Baadhi ya wananchi walitaka huduma za forodha zisogezwe karibu na sehemu wanapoishi.




No comments:
Post a Comment