
Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, Bungeni Dodoma, Mei 5, 2026.
Dodoma
-------------
Bajeti ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 imepanda hadi shilingi trilioni 1.12, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 296 ukilinganisha na shilingi bilioni 898 za bajeti wizara hiyo ya mwaka wa fedha uliopita (2025/2026).
Akiwasilisha hotuba yake ya bajeti hiyo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana Mei 5, 2026. Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, alisema bajeti hiyo imezingatia dira ya taifa kuelekea usalama wa maji na mageuzi ya kiuchumi.
Waziri Aweso alisema wizara imeendelea kuwekeza katika miundombinu himilivu inayoweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua, ikiwemo mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua ili kuimarisha mifumo ya udhibiti wa mafuriko na ukame.
Alitaja baadhi ya kazi za uendelezaji wa rasilimali za maji zinazofanyika kuwa ni kuendeleza ujenzi wa Bwawa la Kidunda kwa gharama ya shilingi bilioni 329.47, ili kuboresha huduma ya maji katika jiji la Dar es Salaam, mikoa ya Pwani na Morogoro ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 47.02.
Nyingine ni kupatikana kwa mkandarasi wa ujenzi wa Bwawa la Farkwa kwa gharama ya shilingi bilioni 312, ili kuboresha huduma ya maji katika jiji la Dodoma na wilaya za Chamwino, Bahi na Chemba.
Pia, kukamilisha ujenzi wa mabwawa ya Gidahababiheg (Hanang’), Malambo na Soitsambu (Ngorongoro); Bugarama na Mwamashindike (Maswa); Nsekwa (Mlele); Kizengi (Uyui); Chikopelo (Bahi); Itaswi (Kondoa); Sengenya (Nanyumbu) na Langai (Simanjiro).
Katika kuboresha huduma ya maji vijijini, alisema miradi 54 yenye vituo vya kuchotea maji 946 imekamilika na inahudumia wananchi 493,932. Kukamilika kwa miradi hiyo kumeongeza upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 83.1 Desemba 2024 hadi asilimia 85.2 Desemba 2025.
Waziri Aweso alisema kukamilika kwa miradi hiyo kumeongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi mijini kutoka asilimia 90.6 Desemba, 2024 hadi asilimia 92.5 Desemba, 2025.
Mradi wa Miji 28
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, utekelezaji wa Mradi wa Maji ya Miji 28 unaendelea na upo kwenye hatua mbalimbali katika miji ya Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Kilwa Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Rujewa, Chunya, Njombe na Makambako.
Pia, katika miji ya Wanging’ombe, Kiomboi, Singida, Manyoni, Mugumu, Chemba, Chamwino, Kasulu, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Chato, Geita, Newala, Nanyamba, Tandahimba, Mtwara, Mafinga, Rorya, Tarime na Songea.
Mradi wa Maji wa Miji 28 unatarajiwa kukamilika Desemba 2026. Aidha, kwa miradi ya Chunya na Singida ambayo imekuwa na changamoto za kimkataba, Serikali ya Tanzania inaendelea na mazungumzo na Serikali ya India ili utekelezaji uendelee.
Vilevile, kwa miradi inayotekelezwa kupitia fedha za ndani katika miji ya Mafinga, Rorya, Tarime na Songea, Waziri Aweso amesema serikali itaendelea kutenga fedha ili kuikamilisha.
Waziri Aweso alisema serikali pia imeendelea kuimarisha huduma za usafi wa mazingira mijini kwa kupanua miundombinu ya majitaka na kuimarisha huduma za uondoshaji majitaka kwa magari maalum ili kudhibiti umwagaji holela, kulinda afya ya jamii, vyanzo vya maji na mazingira.
Ili kuifanya huduma ya usafi wa mazingira kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya miji, serikali inaendelea kutekeleza miradi 26, ikiwemo mtambo wa kuchakata majitaka Mbezi Beach, Dar es Salaam wenye thamani ya shilingi bilioni 70.7 na mabwawa ya kutibu majitaka katika mji wa Babati yenye thamani ya shilingi bilioni 6.9.
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, mwaka wa fedha 2026/27 ni wa kipekee kwa sekta ya maji kwa kuwa Juni 2026, serikali kupitia Wizara ya Maji itafunga rasmi utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, yaani WSDP, iliyoanza mwaka 2006. Kwa miaka 20, WSDP imekuwa siyo tu programu ya miradi, bali injini ya mageuzi ya sekta ya maji nchini.
Kutokana na utekelezaji huo, Waziri Aweso alisema upatikanaji wa huduma ya maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2006 hadi asilimia 85.2 Desemba 2025; na kwa upande wa mijini, huduma imeongezeka kutoka asilimia 73 mwaka 2006 hadi asilimia 92.5 Desemba 2025,
“Mafanikio haya yamepunguza umbali na muda wa kutafuta maji, yamewapunguzia mzigo wanawake na watoto, yameongeza muda wa kufanya shughuli za kiuchumi, yameimarisha afya ya jamii na yameongeza utu wa familia nyingi nchini. Hivyo, WSDP imekuwa programu iliyobadili takwimu za sekta ya maji kuwa mabadiliko halisi katika maisha ya Watanzania,” alisema.
Waziri Aweso alisema serikali imeanza na kuendeleza miradi mikubwa inayogusa maeneo mengi na yenye athari kubwa kwa wananchi, akiitaja kuwa ni pamoja na Mradi wa Maji wa Miji 28, Mradi wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Simiyu, Mradi wa Mto Kiwira, Mradi wa Same–Mwanga–Korogwe, Mradi wa Mugango–Kiabakari–Butiama, Mradi wa Maji Bunda na mabwawa ya kimkakati ya Kidunda na Farkwa.
Katika mwaka 2025/26, wizara imenufaika na fedha za Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa kupata Dola za Marekani milioni 257 kwa ajili ya kutekeleza miradi 15, ikiwemo Mradi wa Bonde la Usangu na Mradi wa Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi katika Mto Mkondoa.
Aidha, Mamlaka za Maji zimepata msaada wa takribani Shilingi bilioni 7 kutoka Serikali ya Ujerumani kupitia Mpango wa IFF-OBA kwa ajili ya miradi ya maji na usafi wa mazingira katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Shinyanga, Bukoba na Arusha.
“Sekta pia imeanza kutumia hati fungani kama chanzo mmbadala cha kugharamia miradi ya maji. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga ilifanikiwa kuuza Hati Fungani ya Kijani yenye thamani ya Shilingi bilioni 53.12 na kukusanya Shilingi bilioni 54.72 sawa na asilimia 103.
“Aidha, wizara inaendelea na maandalizi ya Hati Fungani ya Sekta ya Maji - Water Sector Bond - pamoja na Mkakati wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kuwekeza na kuendesha miradi ya maji,” alisema Waziri Aweso.
Tuzo za Rais Samia
Mafanikio ya sekta ya maji chini ya WSDP yameongeza heshima ya Tanzania kikanda na kimataifa, hiyo inajidhihirisha kwenye kutambuliwa kwa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika masuala ya maji, usafi wa mazingira na ushirikiano wa kimataifa, ambapo Taasisi ya WaterAid ya Uingereza ilimtunuku Tuzo ya kuwa Kinara wa Masuala ya Maji na Usafi wa Mazingira Afrika - The Pan-African Water, Sanitation and Hygiene Champion Award.
“Aidha, kutokana na nchi yetu kuwa kinara katika utekelezaji wa PforR miongoni mwa nchi za Afrika, Benki ya Dunia imeridhia kufadhili Awamu ya Pili ya programu hiyo kwa Dola za Marekani milioni 200,” amesema Waziri Aweso.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akipokea Tuzo.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado zipo changamoto zinazohitaji ufumbuzi ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira nchini. Changamoto hizo ni pamoja na mahitaji makubwa ya kifedha katika miundombinu, usafi wa mazingira; uchafuzi, uharibifu na uvamizi wa vyanzo vya maji; na mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Aweso alisema kwamba katika mwaka wa fedha 2026/27, mwelekeo wa Wizara ya Maji ni kuhakikisha kunakuwa na usalama wa maji kwa ajili ya shughuli za kijamii, lakini pia rasilimali hiyo inakuwa sehemu ya kuchochea mageuzi ya kiuchumi yanayokusudiwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ili kufikia azma hiyo, Wizara ya Maji itaweka msukumo katika kukamilisha maandalizi ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji - National Water Master Plan - ambao utatoa mwongozo wa muda mrefu wa usimamizi, uendelezaji, matumizi na uwekezaji katika rasilimali za maji nchini.
Mpango huo utawezesha sekta kuwa na msingi mmoja wa kupanga miradi mikubwa, kuoanisha mahitaji ya maji ya wananchi na sekta za kiuchumi, pamoja na kuimarisha usalama wa maji kwa kuzingatia ongezeko la watu, ukuaji wa miji, maendeleo ya viwanda, kilimo, mifugo na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wizara pia itaendelea na utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji inayolenga kutumia vyanzo vikuu vya maji, ikiwemo maziwa, mito mikubwa na mabwawa ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma toshelevu ya maji safi na salama, pamoja na kukidhi mahitaji ya sekta za kiuchumi.
Gridi ya Taifa ya Maji ni miongoni mwa vipaumbele katika kufanikisha maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27-2030/31) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) (2025-2030).
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, shilingi trilioni 1.12 zilizoombwa na Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ni kwa ajili ya matumizi ya wizara ili kuiwezesha sekta ya maji kuendelea kuwa injini ya maendeleo nchini.
Wabunge mbalimbali walimpongeza Waziri Aweso na Wizara ya Maji kwa ujumla kwa kazi nzuri, wakisema bajeti hiyo imegusa matumaini ya wananchi katika suala zima la huduma endelevu za maji safi na usafi wa mazingira mijini na vijijini.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment