
Na Christopher Gamaina
Tarime
---------------




Tarime
---------------
Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) kimeendelea kuwa kitovu cha ubunifu na ufanisi katika sekta ya kilimo baada ya kupokea ugeni wa viongozi na wataalamu kutoka mkoa wa Geita waliokwenda kujifunza mifumo bora ya usambazaji pembejeo za kilimo na uendeshaji vyama vya ushirika kwa ujumla.
Ugeni huo ambao ulioongozwa na Katibu Tawala kitengo cha Uchumi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Elphace Msenya, ulijumuisha Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Geita, Meneja wa TFRA Kanda ya Ziwa Mashariki, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale na wataalamu wa kilimo wa halmashauri hiyo.

Ziara hiyo ilifanyika Mei 5, 2026 kwa lengo kuu la kujifunza namna WAMACU Ltd inavyosimamia na kuendesha kwa mafanikio kampuni ya usambazaji wa pembejeo za kilimo, hususan mbolea na mbegu.
Ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea na kujionea miundombinu na miradi mbalimbali inayoendeshwa na ushirika huo, ikiwa ni pamoja na maghala ya kuhifadhi pembejeo za kilimo, mashamba darasa na kiwanda cha kuchakata kahawa.
Aidha, wageni hao walitembelea mradi wa Wakala wa Pembejeo unaosimamiwa na WAMACU Ltd, ambao umeonekana kuwa mfano bora wa jinsi ushirika unavyoweza kurahisisha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Mfumo huo unatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha uchumi wa wakulima wa mkoa wa Mara.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Husna Toni, alieleza kuridhishwa na elimu ya ubunifu, uwazi na usimamizi madhubuti waliyoipata katika ushirika wa WAMACU Ltd.
“Tumekuja kujifunza namna wenzetu wamefanikiwa katika usambazaji wa pembejeo za kilimo ili na sisi tuone namna ya kuwasaidia wakulima wetu ambao wamekuwa hawapati mbolea ya ruzuku kwa wakati,” alisema Husna na kuendelea:
“Tumejifunza namna tutakavyoenda kuanza, wadau ambao tunatakiwa kuwatumia kwenye usambazaji wa mbolea… tumeridhika kabisa - tumefurahi, tumepata maelezo mazuri ambayo tukienda kuyatumia tutapata mafanikio makubwa.”
Husna aliwashukuru viongozi na wataalamu wa WAMACU Ltd akisisitiza kuwa maarifa waliyopata yatasaidia kuboresha utendaji wa vyama vya ushirika na miradi ya kilimo katika mkoa wa Geita.
“Niwashukuru WAMACU wametukaribisha na kutupokea vizuri na wametupa elimu ambayo imetufaa. Elimu hii tutaipeleka kwenye vyama vya ushirika ili viweze kuona namna ya kufanya kazi na kutengeneza mifumu ambayo itavifanya viwe endelevu katika kuwasaidia wakulima wetu,” alisema Husna.
Dkt. Msenya naye aliishukuru WAMACU Ltd akisema wamevuna maarifa yatakayowasaidia kuwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale kuwa na mageuzi makubwa katika masuala ya usambazaji wa pembejeo za kilimo na uendeshaji vyama vya ushirika kwa ufanisi.
“Wananchi wa Nyang’hwale pamoja na shughuli za uchimbaji madini na biashara, kwa ujumla ni wakulima wazuri wa mazao kama mpunga, mahindi na maharage. Kwa hiyo, tumejifunza na kuona mazuri yaliyotendeka hapa WAMACU Ltd ili tuyapeleke kwao.
“Somo tulilotoka nalo hapa WAMACU ni kwamba nguvukazi ya kwanza ni kuwa na watendaji wenye uwezo, yaani kuajiri watu sahihi, ndiyo maana wameweza kutanuka mpaka kuwa na magari yao wenyewe kwa ajili ya kuhudumia wakulima,” alisema Dkt. Msenya.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Kanda ya Ziwa Mashariki, Michael Sanga, alisema “Leo imekuwa siku nzuri kwetu kuja hapa WAMACU Ltd kwa ajili ya kufanya utafiti wa namna nzuri ya kuwapelekea wakulima huduma kwa ufanisi.”
Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji wa WAMACU Ltd, Olais Piniel Siray, alisema wao kama ushirika wamefurahishwa na ujio wa wageni hao kutoka Geita.
“Waliona WAMACU Ltd kama sehemu sahihi ya kuja kujifunza baada ya kusikia sifa zetu kwamba ni chama ambacho kimefanikiwa kwa hatua kubwa,” alisema Meneja Olais.
Aliendelea: “Wamepata mafunzo kama darasa kutoka kwa wataalamu wetu wa ndani na baadaye tukaenda kutembelea maeneo ambayo walihitaji. Sisi tunachukulia hii kama sehemu ya mafanikio na inatupa fursa ya kuitangaza WAMACU Ltd ndani na nje ya nchi.”

Naye Makamu Mwenyekiti wa WAMACU Ltd, Emmanuel Ndege Benson, alisema “Wamejifunza, wamefurahia namna tunavyotoa huduma na wameahidi kwenda kufikisha elimu hiyo kwa wakulima wao.”
WAMACU Ltd ni miongoni mwa vyama vikuu vya ushirika vilivyopewa kusimamia usambazaji wa mbolea za ruzuku ya serikali kwa wakulima kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), TFC na OCP.
Aidha, kwa sasa ushirika huo wa WAMACU Ltd una leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo, ikiwemo mbolea kutoka TFRA.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment