
Meneja Miradi wa FZS Kanda ya Serengeti, Masegeri Rurai (katikati mbele) na Afisa Uhifadhi wa Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Robert Masobeji (kushoto mbele), wakikabidhi msaada wa vifaa vya kisasa katika Chuo cha VETA Ngorongoro (NVDTC), JANA Mei 4, 2026.
Akiripoti kutoka
Ngorongoro
-----------------
Chuo cha VETA Ngorongoro (NVDTC) kilichopo kata ya Samunge katika wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha kimenufaika na msaada wa vifaa vya kisasa vyenye thamani ya shilingi milioni 85 kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Msaada huo ulikabidhiwa kwa chuo hicho Mei 4, 2026 na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja Mradi wa FZS Kanda ya Serengeti, Masegeri Rurai, alitoa wito kwa jamii ya Ngorongoro kuwekeza kwenye elimu ili kuendana mabadiliko ya kiuchumi kwa ajili ya uhifadhi endelevu.
"Hakuna namna, lazima tubadilishe mfumo wa maisha yetu kupitia elimu. Ardhi haitoshi, tuwape vijana wetu elimu, na wanaohitimu elimu ya sekondari waje wapate mafunzo katIka chuo hiki. Miradi tunayojenga inataka mafundi ambao ni vijina wetu,” alisisitiza Rurai ambaye ni mmoja wa wahifadhi wakongwe katika ikolojia ya Serengeti.
Rurai alitumia fursa hiyo pia kuishukuru Benki ya KfW kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za uhifadhi na maendeleo ya jamii kupitia FZS na TANAPA.
Naye Afisa Uhifadhi wa Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Robert Masobeji, aliishikuru Benki ya KfW na FZS kwa kutoa msaada wa vifaa hivyo.
"Niwapongeze FZS, KfW kwa kazi iliyofanyika hapa [NVDTC] na kwa kuendelea kufanya kazi katika shughuli za uhifadhi na maendeleo ya jamii,” alisema Masobeji ambaye alimwakilisha Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti katika hafla hiyo.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Ngorongoro, Fredrick Laizer, aliishukuru FZS kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha utoaji wa mafunzo ya ufundi chuoni hapo.
"Niwashukuru FZS kwa namna ambavyo wamechangia elimu hapa chuoni, mpaka sasa wamefadhili wanafunzi 67 na vifaa mlivyotuletea ni vingi. Hii ni zaidi ya fedha, ni vifaa vya kisasa na baadhi ya vyuo watakuja kuazima hapa kwetu,” alisema Laizer.
Wanafunzi wa chuo hicho waliahidi kutumia vifaa hivyo viuri k ili waweze kuiva zaidi katkka mafunzo wanayopata chuo hapo.
"Tunashukuru sana wafadhili wetu (KfW, FZS na TANAPA) kwa msaada wa vifaa hivi walivyotupatia leo. Mimi ni mmoja wa wanafunzi wanaofadhiliwa kusoma hapa na hakika ninayaona matunda ya uhifadhi,” mmoja wa wanachuo, Anna Balikeri Jacob, alisema.
Nao wananchi wa kijiji cha Samunge pia walishukuru KfW, FZS na TANAPA kwa kutoa msaada wa vifaa hivyo, huku wakitoa wito kwa vijana kutumia fursa hiyo kuwa mabingwa wa fani wanazosoma.
"Sisi zamani hatukupata fursa kama hizi, wanafunzi sasa someni kwa bidii na tunawashukuru sana FZS, KfW na TANAPA kwa kuletea watoto wetu vifaa vya kisasa,” alisema Mesia Richi, mmoja wajumbe wa Serikali ya Kijiji hicho cha Samunge.

Mapokezi ya Meneja Miradi wa FZS Kanda ya Serengeti, Masegeri Rurai, katani Samunge.
FZS ni ShirIka la Uhifadhi la Kimataifa lenye makao makuu nchini Ujerumani, ambalo limekuwa likisaidia Serikali ya Tanzania katika kuimarisha masuala ya uhifadhi, huku uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti ukiwa moja ya vipaumbele vyake kwa kwa miaka mingi sasa.


No comments:
Post a Comment