
Nicolaus Mahando Mgaya "Chichake"
Na Mwandishi Wetu
---------------------------
Mdau wa maendeleo ya jamii, Nicolaus Mahando Mgaya - maarufu kwa jina la Chichake, ameongoza harambee ya kuchangia maendeleo ya Kanisa Katoliki Parokia ya Sirari na kufanikisha upatikanaji wa shilingi zaidi ya milioni 30.
Chichake ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kemanyanki Contractors Manpower and Supply, alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo iliyofanyika jana Mei 10, 2026 katika kanisa hilo lililopo wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Harambee hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, waumini na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya mji wa Sirari uliopo mpakani na nchi ya Kenya.
“Harambee yetu imekuwa ya mafanikio, tumepata shilingi milioni 30 kwa ajili ya maendeleo ya kanisa,” Chichake aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara baada ya harambee hiyo kumalizika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, kiasi hicho cha fedha kitasaidia kuimarisha huduma za kiroho na miundombinu ya kanisa hilo.
Chichake alisema maendeleo ya taasisi za dini ni msingi muhimu katika kujenga jamii yenye maadili, mshikamano na matumaini kwa kizazi cha sasa na vijavyo.
Aliongeza kuwa huduma za kiroho zina mchango mkubwa katika malezi na ustawi wa jamii, hivyo ni wajibu wa kila mwenye uwezo kushiriki kwa vitendo kuhakikisha zinaendelea kuwa imara.
Uongozi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Sirari ulimpongeza na kumshukuru Chichake kwa moyo wake wa kuwa tayari kujitolea kuchangia maeendeleo ya jamii.
“Huu ni mfano wa moyo wa kujitolea, mshikamano na upendo kwa jamii,” ulisema uongozi huo.
Aidha, mafanikio ya harambee hiyo yalipokewa kwa furaha na waumini, wakieleza kuwa hatua hiyo imechochea matumaini ya maendeleo ya kanisa hilo.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment