NEWS

Sunday, 10 May 2026

Mahusiano ya Mgodi wa Barrick North Mara na jamii inayouzunguka yaimarika zaidi


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
----------------------------

Hali ya mahusiano kati ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyo jirani imeimarika zaidi kwa sasa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Lakini pia, matukio ya uvamizi yaliyokuwa yakifanywa na makundi ya watu wanaojulikana kama ’intruders’ katika mgodi huo yanaelekea kuwa historia.

“Mahusiano ya Mgodi wa North Mara kwa sasa ni mazuri na hata matukio ya uvamizi mgodini yamepungua hadi wastani wa mtu mmoja kwa siku,” Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwambia waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni.

Meja Gowele alibainisha kuwa matukio ya kujaribu au kuvamia mgodi huo ili kuiba mawe yenye dhahabu yamepungua kutoka watu 100 kwa siku mwaka 2020 hadi wastani wa mmoja kwa siku hivi sasa.

“Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2020 watu zaidi 100 walikuwa wakivamia mgodi lakini kwa sasa ni wastani wa mtu mmoja kwa siku,” alisema.

Alisema mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa mahusiano kati ya jamii na mgodi pamoja na faida za moja kwa moja zinazotokana na uwekezaji wa kampuni ya Barrick ambayo inaendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Alitaja baadhi ya faida hizo kuwa ni fursa nyingi za ajira kwa wazawa katika kampuni ya Barrick pamoja na wakandarasi wazawa wanaopata fursa za kibiashara katika mgodi huo.

“Ajira kwa wazawa zimekuwa nyingi sio tu kutoka Barrick bali pia kutoka kwa wakandarasi wa mgodi ambao wengi wao pia ni wazawa na wanatoa ajira nyingi kwa vijana,” alifafanua kiongozi huyo.

Aidha, Meja Gowele alisema utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na mabilioni ya fedha zinazotolewa kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wa Barrick North Mara umechochea kuimarika kwa mahusiano baina ya mgodi huo na jamii.

Aliongeza kuwa fedha za mrabaha zinazotolewa na mgodi huo kwa vijiji pia zimechangia kuwepo kwa mabadiliko chanya ya kimaendelo na mahusiano bora kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka.

“Wananchi wanaona fedha za CSR na mrabaha zinavyojenga miradi ya maendeleo kwenye vijiji, unakuta kijiji kimoja kina shilingi bilioni 1.7 na zinatekeleza miradi.

“Kwa hivyo, wananchi wanaona mgodi una faida kwao. Mwanzoni walikuwa wanaona mgodi ni adui lakini sasa hivi wanauona ni rafiki - hawataki uondoke,” alisema Meja Gowele.

Mkuu huyo wa wilaya alipongeza kazi kubwa inayofanywa na mgodi huo kupitia Idara ya Mahusiano ambayo alisema imesaidia kuimarisha mahusiano kati ya mgodi huo na vijiji vilivyo jirani.

“Idara ya Mahusiano imefanya kazi kubwa na nzuri, sasa hivi mgodi ni rafiki wa wananchi na mahusiano ni mazuri,” alisema Meja Gowele.

Pia, aliwapongeza wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo kwa ushirikiano wanaotoa katika kuimarisha mahusiano na mgodi kwa manufaa ya pande zote mbili [mgodi na jamii].

Hata hivyo, Meja Gowele alisema zipo changamoto zinazohusiana na suala la fidia ambazo zinaendelea kutafutiwa uvumbuzi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages