
Katibu wa Halmashauri Kuu CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, akizungumza alipotembelea na kukagua utekelezaji Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Tarime na Rorya, leo Mei 15, 2026.
Mara Online News
Tarime
-------------


(Picha zote na Mara Online News)
Tarime
-------------
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Tarime na Rorya.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 134, ukiwa ni moja ya miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa katika mkoa wa Mara.
Akizungumza leo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha usambazaji maji cha Mogabiri kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Kihongosi amewapongeza wakandarasi kwa usimamizi na ujenzi wa mradi huo.

"Niwapongeze wakandarasi kwa usimamizi na ujenzi wa mradi vizuri, niwahakikishie nitafikisha salamu kwa Waziri wa Maji kwamba mradi ni mzuri, fedha nyingine ya kutosha iletwe hapa kazi ikamilike, wananchi waanze kupata maji safi na salama,” amesema.
Mradi huo ukikamilika utawezesha maelfu ya wananchi wa wilaya za Rorya na Tarime kuanza kufuharia huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria.
Hivyo, Kihongosi ametumia fursa hiyo pia kuwahimiza wananchi kulinda miundombinu ya maji kwani ikiharibika au kuharibiwa gharama ya ukarabati itapunguza kasi ya ujenzi wa miradi mingine ya maendeleo nchini.
"Niwaombe watu wa Mara, watu wa Tarime, miradi hii ilindwe kwa sababu ni kodi za wananchi, ni miradi yetu, ni mali yetu,” amesisitiza.
Aidha, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, kwa kuiwakilisha vizuri serikali katika usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
“Tuzidi kuwa na imani na serikali na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tushirikiane katika ajenda zote za maendeleo,” ameongeza Kihongosi.

(Picha zote na Mara Online News)
Awali, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Rorya, Mhandisi James Kishinhi, amemweleza Kihongosi kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba 2026.
"Ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia 18, mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 29, anadai bilioni nane, lakini mwezi wa tano amelipwa bilioni 1.6 ili aweze kurudi 'site' na kuendelea na kazi.
"Mpaka sasa, tumeshajenga chujio la kusafisha na kutibu maji kiasi cha lita milioni 29 kwa siku,” alisema Mhandisi Kishinhi.
Katika ziara hiyo, Kihongosi aliambatana na viongozi wengine mbalimbali wa CCM na Serikali katika mkoa wa Mara, wakiwemo kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA).
No comments:
Post a Comment