NEWS

Monday, 18 May 2026

Mbunge Waitara alia na madhila wanayopata wananchi wa Tarime Vijijini kutoka Hifadhi ya Serengeti



Mbunge wa Jimbo la Tarime, Mwita Waitara, akizungumza Bungeni jijini Dodoma.

Na Mwandishi Maalumu
Dodoma
--------------

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara, Mwita Waitara, ameishukia vikali Wizara ya Maliasili na Utalii, akihoji uhalali wa kuthamini mapato yatokanayo na utalii huku wananchi wanaopakana na hifadhi za wanyamapori ‘wakiumia’.

Amesema madhila yanayosababishwa na wanyamapori waharibifu na wakali kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyo jirani na hifadhi, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti inayopakana na jimbo lake ‘hayahesabiki’.

Waitara alipaza sauti hiyo Bungeni jijini Dodoma, Ijumaa iliyopita, wakati akichangia Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, huku akitaja magumu ambayo wapigakura wake wanapitia kuwa ni pamoja na kuvamiwa na tembo, kutaifishwa mifugo na wengine kupotea.

“Hapa [bungeni] hiki mimi ni kipindi cha tatu, nitakayozungumza hapa nimeyazungumza tangu mwaka 2025, majibu hayajaweza kupatikana, tunazungumza mapato ya nje, lakini tunazungumza maisha ya watu wetu.

“Mtu anapokwambia tembo ameua huyu ni mtu ameuawa, pengine angeweza kuwa kama Waitara - angeweza kuwa mbunge, angeweza kuwa waziri, aliyekanyagwa na tembo na huyu ambaye ameliwa na mamba,” alisema Waitara.

Aidha, mbunge huyo alieleza kutoridhishwa na mchango wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kama si Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa maendeleo ya huduma za kijamii katika vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo.

“Tarime Vijijini mimi nimepakana na Hifadhi ya Serengeti, habari ya CSR (Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii) ukienda pale Kwihancha hawana maji, hawana barabara, hakuna vifaa vya shule na kwenye hospitali lakini kuna Hifadhi ya Serengeti pale.

“Nenda kata ya Gorong’a hakuna kituo cha afya, hakuna madarasa, mchango wao ni nini pale? Nenda kata ya Nyanungu CSR ya pale haieleweki - haina formula, yeye anaweza akaamua ajenge darasa moja - asijenge, alisema Mbunge Waitara.

Pia, aliilaumu TANAPA akidai imeshindwa kufadhili uchimbaji wa malambo maji kwa ajili ya mifugo katika vijiji vya jimbo la Tarime Vijijini vinavyopakana na Hifadhi ya Serengeti, hali inayochangia migongano isiyoisha baina ya pande hizo mbili.

“Wakati wa kiangazi hakuna maji, wameshindwa kuchimba malambo pale, mfugaji analazimika kuchukua mifugo akainyweshe maji karibu na hifadhi, akikamatwa anataifishwa ng’ombe zake, akikamatwa anapigwa,” alisema.

Kwa upande mwingine, Waitara alizitupia lawama wizara husika kwa kuchelewesha utatuzi wa mgogoro wa muda mrefu wa kugombea ardhi kati ya Hifadhi ya Serengeti na vijiji vinavyoizunguka Tarime Vijijini.

“Kuna mgogoro wa ardhi, mwaka 2021 mawaziri wanane walienda Tarime Vijijini, walipofika pale katika vijiji saba kwa maana ya Kwihancha, Gorong’a, Nyanungu. Kuna GN ya mwaka ’68.

“Kilichofanyika, eti mawaziri wameenda pale, badala ya kuwasikiliza wananchi ambao wanaishi lile eneo, hifadhi ndiyo inawaonesha beacons (vigingi), walikuwa wanapindisha… mpaka leo wameacha pale kiporo, hizi GN wananchi wanazijua, wamekaa pale miaka zaidi ya 100.

“Naomba mgogoro wa Tarime Vijijini na Hifadhi ya Serengeti - vijiji saba twende, wako wazee wenye miaka 70, miaka 80, wamezika pale, wamezaliwa pale, twende tupitie beacon moja baada ya nyingine.

“Huwezi kutatua mgogoro wa wananchi huwasikilizi wananchi - mhifadhi ndiye anakupa mipaka, waziri unapiga makofi halafu unaondoka, hapana. Twende tufanye shirikishi,” alisema Waitara.

Kutokana na hali hiyo, Waitara alishauri Wizara za Ardhi, Maliasili na Utalii, Mifugo, Kilimo, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zishirikiane kutafuta suluhisho la mgogoro huo ili kuwapa tabasamu wananchi husika.

“Migogoro iliyopo ni mingi, nitaomba wabunge ambao tuko karibu na hifadhi hizi na misitu tupate muda tuzungumze tuiambie serikali wafanye nini ili watu wetu wasiendelee kuumia,” alisema na kuendelea:

“Kila bunge watu wanalalamikia hifadhi, kila bunge watu wanasema migogoro, unazungumza hapa mamba, tembo, yaani ni vurumai, haiwezi kuwa hivyo. Tunapopenda watalii tunapenda fedha tupate maendeleo, lakini lazima tuangalie pia ustawi wa watu wetu.

“Hivi kweli katika hali ya kawaida, watu wako hawana sehemu ya kulima, watu wako hawana sehemu ya kuishi, wewe unazungumza habari ya wanyama. Ndiyo ni muhimu, kipi ni muhimu kati ya binadamu na wanyama.

“Hayo manufaa ya maliasili ni wananchi hawa hawa, serikali ifunguke, mawaziri wafunguke tu, wabunge wana migogoro mingi, waziri atuite kikao tuzungumze naye, twende kwenye majimbo tutafute suluhu,” alisisitiza Mbunge Waitara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages