NEWS

Friday, 8 May 2026

Mfanyabiashara Mtanzania Nyambari Nyangwine, wafanyabiashara wa nchini Uturuki wajipanga 'kuteka' masoko ya kimataifa




Na Mwandishi Wetu

Mfanyabiashara Mtanzania, Nyambari Nyangwine, amehudhuria maonesho makubwa ya mashine za ujenzi katika jiji la Konya nchini Uturuki, ambapo alipata mwaliko maalum kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa jiji hilo.

Maonesho hayo ya aina yake yamefanyika Mei 8, 2026 katika jiji la Konya ambalo ndilo mkoa mkubwa na lenye viwanda vingi zaidi nchini Uturuki.

Ziara hiyo ya Nyangwine imefungua ukurasa mpya wa majadiliano ya kimkakati kati yake na wawekezaji wa Uturuki, ambapo mazungumzo yao yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, teknolojia, kilimo, ajira na elimu ya kitaalamu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhudhuria maonesho hayo, Nyangwine ametaja baadhi ya mambo muhimu waliyojadiliana kuwa ni kushirikiana kuanzisha kongani ya viwanda nchini Tanzania.

Amefafanua kuwa hatua hiyo inalenga kushirikiana na wawekezaji kutoka jiji la Konya kutumia fursa ya Bandari ya Dar es Salaam kama lango la biashara kwa nchi jirani, zikiwemo Rwanda, Burundi na Zambia.

“Mambo muhimu tuliyoongea ni ushirikiano wa kuanzisha kongani ya viwanda nchini Tanzania ili kutumia fursa ya Bandari ya Dar es Salaam kukamata masoko ya nchi za jirani kama Rwanda, Burundi na Zambia,” amesema Nyangwine.

Nyangwine amesema pia wamejadiliana kuhusu Teknolojia ya Habari (IT), ambapo wameonesha dhamira ya kushirikiana katika kuwaendeleza wataalamu wa Kitanzania, wakiwemo wanafanyakazi wa kampuni zake.

Katika sekta ya kilimo, amesema wamekubaliana kuangalia fursa za kuongeza thamani mazao ya kilimo kabla ya kuyapeleka katika masoko ya kimataifa ili kuongeza mapato kwa wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Aidha, masuala ya ajira pia yalikuwa sehemu ya mazungumzo yao, ambapo Nyangwine amesisitiza umuhimu wa kufungua nafasi zaidi kwa vijana wa Kitanzania kupitia uwekezaji wa pamoja na programu za mafunzo ya kitaalamu.

Kwa upande wa elimu, amesema wamejadili ushirikiano wa kuandaa wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kuandika vitabu vya kitaalamu katika nyanja mbalimbali ili kukuza maarifa, tafiti na uzalishaji wa maudhui bora ya elimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages