
Diwani wa Kata ya Rabuor Gerald Samwel Ng'ong'a, akikabidhi cheti cha pongezi kwa mtumishi wa sekta ya afya katani hapo wakati wa sherehe za Mei Mosi, jana.
Rorya
--------------
Diwani wa Kata ya Rabuor katika wilaya ya Rorya mkoani Mara, Gerald Samwel Ng'ong'a, ameahidi kufanya mageuzi kwenye sekta ya elimu katani hapo kwa kuanzisha Kituo cha Rasilimali za Walimu (TRC).
Amesema hatua hiyo itahusisha kufunga mtambo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kusaidia walimu 26 wa shule za msingi watakaojiunga na Chuo cha Utalii Musoma kusoma diploma kwa njia ya masafa.
![]() |
| Diwani Ng'ong'a (katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na watumishi wa afya |
Ng’ong’a alitoa ahadi hiyo wakati wa tukio la kusherehekea Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) katani hapo jana, ambalo lilihudhuriwa na wananchi mbalimbali, wakiwemo wafanyakazi na wanafunzi.
"Nilishawaza kuanzisha kituo cha TRC, nimepata eneo Nyakoba na nimeagiza lisajiliwe, kitakuwa na huduma za kidijitali na maktaba,” alisema Ng’ong’a na kuendelea:
“Lengo ni kuhakikisha wanafunzi na walimu wanapata 'access', kutakuwepo na 'mentor teachers' kulingana na masomo mbalimbali, programu ya TEHAMA na 'Smart Interactive Board' ili tufanye vizuri.
![]() |
| Diwani Ng'ong'a (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi wanafunzi wa sekondari na viongozi. |
"Rabuor tumewasha moto kwa walimu wa Kiingerza na Hisabati, tumewasha moto kwa 'competence and technics' kwa walimu wanao- upgrade kutoka certificate (cheti) kwenda diploma, nitawalipia asilimia 20 ya milioni moja.”
Hivyo, Diwani Ng’ong’a ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo aliwaomba wadau wa elimu kumuunga mkono katika hatua hiyo ya kuwezesha walimu wa shule za msingi ndani ya kata hiyo kupanda kitaaluma kutoka ngazi ya vyeti hadi diploma na kuendelea.
"Umoja ni nguvu, anzisheni timu na klabu za ufundishaji, yapo yatakayohitaji uwezesho tuambizane, kila shule kuwepo na mtihani mmoja kwa mwezi pamoja na 'monthly joining test' kwa shule zote za msingi na sekondari,” alisema.
Kwa upande wa sekta ya afya, diwani huyo alisema atashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuona namna ya kuwapa motisha wahudumu ngazi ya jamii ili kuboresha zaidi huduma za afya katika kata hiyo.
![]() |
| Diwani Ng'ong'a akigawa rimu |
Sherehe hizo zilifanyika sambamba na tuzo mbalimbali kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu - kwa kuwapa katoni 10 za rimu, ngao za heshima kwa shule zilizofanya vizuri, vyeti na fedha taslimu kwa walimu waliofaulisha wanafunzi kwa alama A katika masomo ya Hisabati na Kiingereza.
Afisa Elimu Kata ya Rabour, Mwalimu Aprijanus Israel Katoto, alimpongeza Diwani Ng'ong'a kwa namna anavyojizatiti kushirikiana na watumishi wa umma katika kata hiyo.
"Nimpongeze kwa namna anavyounganisha watumishi wa kata yake, kila shule ameipa zawadi. Sherehe hizi ni sehemu tunayokutana na kufurahi pamoja na kuwasilisha changamoto zetu kwa viongozi ili zipatiwe ufumbuzi,” alisema Mwalimu Katoto.
![]() |
| Diwani Ng'ong'a (wa pili kulia waliokaa) katika picha ya pamoja na watumishi wa sekta ya elimu. (Picha zote na Mara Online News) |




No comments:
Post a Comment