
Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema limefikia makubaliano na Serikali ya Tanzania yatakayowezesha kupatikana kwa ufadhili wa dola milioni 375.5, huku nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikikabiliana na athari za vita ya Marekani dhidi ya Iran.
Jopo la maafisa wa ngazi ya juu wa IMF likiongozwa na Nicolas Blancher, lilifanya ziara rasmi nchini Tanzania na kufanya mazungumzo kuhusu awamu ya sita na saba ya ufadhili wa shirika hilo kwa Tanzania.
Kufuatia ziara hiyo, jopo hilo limependekeza ufadhili wa dola milioni 375.5 kwa Tanzania.
Pendekezo hilo sasa linasubiri idhinisho kutoka kwa Kamati Kuu ya Utendeji ya IMF kabla ya fedha hizo kutolewa, na kufikisha jumla ya ufadhili wa shirika hilo kwa Tanzania kufikia dola milioni 1,052.
IMF imesema malengo ya miradi yake nchini Tanzania yameafikiwa.
Ripoti hiyo imesema ukuaji wa uchumi nchini Tanzania umesalia kuwa dhabiti, huku mfumuko wa bei nao ukisalia kuwa chini na imara.
Aidha, IMF imesema Tanzania ina hazina ya kutosha ya fedha za kigeni mbali na kuwa bajeti ya elimu na afya imeongezeka pakubwa.
Hata hivyo, Tanzania imekumbwa na matatizo ya kiuchumi tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Bei ya mafuta imepanda na kumekuwa na upungufu mkubwa wa pembejeo, kama vile mbolea ya kilimo.
Blancher, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuruhusu ongezeko la bei za mafuta kwenda kwa bei za ndani na kwa kuruhusu kiwango cha ubadilishaji wa fedha za kigeni kuamuliwa na mahitaji na upatikanaji.
IMF imesema inatarajia uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 5.9 mwaka huu, huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kupanda hadi asilimia 4.7.
IMF hata hivyo, imeonya kuwa kupanda kwa bei ya mafuta na mbolea na kutatizwa kwa usafiri wa anga na usambazaji wa bidhaa dunia huenda kukawa na athari kubwa kwa sekta za kilimo, utalii na usafiri na hivyo kuchangia pakubwa mfumuko wa bei ya bidhaa.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment