
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
--------------
Dodoma
--------------
Wakulima nchini wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa pembejeo bora, uendelezaji wa mnyororo wa thamani wa zao la chikichi, biashara na masoko ya mazao mbalimbali ya kilimo kimataifa.
Hayo yalibainishwa katika Kikao cha Nne cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo baina ya Tanzania na Indonesia (4th Joint Agriculture Cooperation Committee - JACC) kilichofanyika jijini Dodoma wiki iliyopita, kikilenga kukuza sekta ya kilimo na uchumi wa pande zote mbili.
Kikao hicho, pamoja na mambo mengine, kilijadili uimarishwaji wa ushirikiano katika uzalishaji wa mbolea ili kukidhi mahitaji ya yanayokadiriwa kufikia tani 1,200,000 kwa mwaka 2026/2027 na kupunguza uingizwaji wa mbolea kutoka nje ya nchi.
Aidha, kikao hicho kilijadili upatikanaji wa mafuta kwa kuongeza uzalishaji wa chikichi, kuimarisha utafiti na teknolojia katika zao hilo, kuongeza uzalishaji wa miche bora na kubadilishana teknolojia baina ya Tanzania na Indonesia.
Ushirikiano huo unaendelea hadi sasa kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Mkindo kilichopo mkoani Morogoro.
Kikao hicho ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Indonesia katika kilimo, ambapo kikao cha tatu cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo cha November 2014, kilijikita katika kukuza ushirikiano, maendeleo ya tafiti zana za kilimo na upatikanaji wa masoko.
No comments:
Post a Comment