NEWS

Thursday, 14 May 2026

Waziri Mavunde asimamisha uchimbaji wa madini kwenye mto




Na Mwandishi Wetu
Katavi
------------

Kufuatia ukaguzi uliofanywa kwa wamiliki wa leseni wanaofanya uchimbaji wa madini kwenye mto na kuathiri mazingira, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameatoa maelekezo ya kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji huo mkoani Katavi.

Waziri Mavunde alitoa kauli hiyo Mei 13, 2026 alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za uchimbaji madini katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi.

"Mhe. Rais ametupa maelekezo mahsusi Wizara ya Madini kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika kwa mujibu wa Sheria na zisilete athari kwenye mazingira. Tumeshuhudia sote kinachofanyika hapa ni kinyume na matakwa ya Sheria yetu ya Madini Sura 123," alisema Waziri Mavunde.

Aliendelea: "Hivyo, naelekeza kuanzia leo shughuli zote za uchimbaji zisimame mpaka pale mtakapotekeleza wajibu wenu kama mlivyoelekezwa na Afisa Madini Mkazi wa Katavi kupitia barua aliyowaandikia. Pia, wamiliki wa leseni wasilisheni mpango wa kuhifadhi mazingira kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji tena."

Vilevile, Waziri Mavunde alifanya ukaguzi wa mikataba ya msaada wa kiufundi (TSA) waliyoingia wachimbaji wadogo wa kitanzania na wawekezaji wa nje na kubaini mapungufu yaliyosababisha kuiagiza Ofisi za Afisa Madini Wakazi wa Mikoa ya kimadini kufanya ukaguzi wa mikataba hiyo nchi nzima ili kubaini iwapo inawanufaisha Watanzania na inazingatia matakwa ya kisheria.

Akieleza utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa maeneo ya uchimbaji, Waziri Mavunde alitoa maelekezo kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kutoa Hati ya Makosa (Default Notice) kwa wamiliki wote wa leseni za utafiti wasioendeleza na kufuata masharti ya leseni hizo.

"Lengo ni kuyafuta maeneo yote ya leseni za utafiti yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo kupitia vikundi vyao. Aidha, maeneo mengine yatatumika kugawa maeneo kwa wachimbaji wadogo vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia programu ya Mining for A Brighter Tomorrow (MBT)," alibainisha Waziri Mavunde.

Akibainisha juu ya leseni alizozifuta mwezi uliopita, Waziri Mavunde alitangaza kutenga leseni tatu za utafiti ili zigawiwe kwa wachimbaji wadogo mkoani Katavi, ambapo wachimbaji wadogo walishukuru na kupongeza jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa wakati.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages