NEWS

Sunday, 17 May 2026

Utekelezaji Mradi wa Barrick-Twiga wa kuboresha elimu nchini wafikia asilimia 83



Meneja Mkazi wa Barrick Tanzania, Dkt. Melkiory Ngido (aliyevaa skafu), akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Sekondari Nyang’hwale.

Na Mwandishi Wetu
Nyang’hwale
-------------------

Utekelezaji wa mradi wa kujenga miundombinu ya shule za sekondari nchini unaojulikana kama ‘Barrick-Twiga Future Forward Education Program’, unaotekelezwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania, umefikia asilimia 83.

Kwa mujibu wa Meneja Mkazi wa Barrick Tanzania, Dkt. Melkiory Ngido, mradi huo unaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa awamu ya pili iliyoanza Machi 2025.

Amesema tayari takriban shilingi bilioni 19 zimeshatolewa - sawa na asilimia 79 ya bajeti ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 318, mabweni 116 na vyoo 542 katika shule 65 nchini.

Aidha, awamu ya kwanza ya mradi huo iliyoanza Julai 2023 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 10, ilinufaisha shule za sekondari 64 nchini kupitia ujenzi wa vyumba vya madarasa 396, mabweni 97 na vyoo 600.

Dkt. Ngido alisema hayo juzi katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mabweni mawili, vyumba vitano vya madarasa na vyoo matundu manane katika Shule ya Sekondari Nyang’hwale iliyopo wilaya ya Nyang’hwale, mkoani Geita.

Alisema Barrick itaendelea kushirikiana na serikali katika kuchochea maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali, hususan sekta ya elimu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Machi 2023, Barrick iliahidi kutoa dola za Marekani milioni 30 sawa na shilingi bilioni 70.5 kuunga mkono ajenda ya Serikali ya Tanzania ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Mpango wa ‘Barrick-Twiga Future Forward Education Program’ ni kujenga vyumba vya madarasa 1,090, mabweni 270 na matundu ya vyoo 1,640 katika shule 161 nchini kote, vitakavyohudumia takriban wanafunzi 49,000.

Lengo ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kusoma katika shule za serikali ambao walikuwa wanakosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na upungufu wa miundombinu, lakini pia kuhakikisha wanapata elimu katika mazingira rafiki.

Dkt. Ngido aliyasema mradi huo utawezesha na kuongeza nafasi za wanafunzi kujifunzia katika mazingira bora zaidi, kupunguza msongamano madarasani, kuimarisha mazingira ya malazi kwa wanafunzi, hususan wa kike na kuboresha usafi, afya na hadhi ya shule kwa ujumla.

Aliongeza kuwa Barrick-Twiga inaamini kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla, na kwamba taifa lolote linalotaka kujenga uchumi imara, jamii yenye maarifa na kizazi chenye ushindani halina budi kuwekeza kwa makusudi katika elimu.

Dkt. Ngido akizungumza katika hafla hiyo

Kuhusu ujenzi wa mabweni mawili, vyumba vitano vya madarasa vitano na vyoo matundu manane katika Shule ya Sekondari Nyng’hwale, Dkt. Ngido alisema ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 401.8.

“Leo hatujaja kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi pekee; tumekuja kushuhudia uthibitisho wa dhamira ya pamoja kati ya serikali na sekta binafsi katika kuwekeza kwenye elimu, ustawi wa jamii na mustakabali wa watoto wa Tanzania.

“Tunafahamu kuwa darasa bora hujenga ufaulu bora. Bweni salama hujenga utulivu wa mwanafunzi. Mazingira safi hulinda afya, heshima na hadhi ya mtoto wa Kitanzania. Hivyo basi, tunapojenga miundombinu ya elimu, tunakuwa tunajenga ndoto, uwezo, fursa na maisha ya baadaye,” alisema Dkt. Ngido.

Aliwapongeza wanafunzi watakonufaika na miundombinu hiyo akisema “Miundombinu hii mnayoiona leo ni ujumbe kwamba taifa linaamini ndani yenu wanafunzi. Tumia fursa hii vizuri. Jifunzeni kwa bidii, muwe na nidhamu na mjenge maisha yenu kupitia elimu.”

Dkt. Ngido alitumia nafasi hiyo pia kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ushirikiano wa maendeleo. “Barrick-Twiga inatambua na kuthamini juhudi kubwa za serikali katika kuimarisha sekta ya elimu. Sisi tunajivunia kuwa sehemu ya safari hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyang’hwale, Kaunga Amani, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wa nje na ndani.

Kupitia uwekezaji, wananchi wanaendelea kunufaika kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini kote, hususan katika sekta za elimu, afya, maji safi na ujenzi wa miundombinu bora ya barabara.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Husna Toni, aliishukuru Barrick Tanzania kwa mchango mkubwa uliowezesha ujenzi wa miundombinu hiyo ambao itasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuwawezesha kusoma katika mazingira rafiki.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages