NEWS

Friday, 1 May 2026

Wazee mashuhuri, viongozi wa dini Tarime wasifu ripoti ya Jaji Chande



Kutoka kushoto ni Chifu wa Watimbaru, Peter Zakaria, Mwenyekiti wa Koo 12 za Wakurya Wilaya ya Tarime, Mwikwabe Makame, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Mara, Joseph Nyiraha na Sheikh wa BAKWATA Nyamwaga, Khalifan Mtongori.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Baadhi ya wazee mashuhuri na viongozi wa dini wilayani Tarime, Mara, wameeleza kupokea kwa mtazamo chanya ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Wakizungumza na Mara Online News kwa nyakati tofauti leo, walisema ripoti hiyo imeonesha mambo ambayo serikali ikiyafanyia kazi yataimarisha amani na mshikamano wa kitaifa.

“Ile ripoti hata sisi wazee tunaiunga mkono, imeweka mambo wazi,” alisema Mwenyekiti wa Mila wa Koo 12 za Kabila la Wakurya katika Wilaya ya Tarime, Mwikwabe Makabe.

Chifu wa Koo ya Watimbaru ya Kabila la Wakurya Wilaya ya Tarime, Peter Zakaria, alisema kilichoelezwa kwenye ripoti ya Tume ya Uchunguzi ndicho kilichotokea wakati na baada ya Oktoba 29, 2026.

"Ripoti ni nzuri sana, waliifanya kiumakini, jinsi walivyoitoa ndivyo jinsi ilikuwa kipindi cha vurugu. Mtu anatuma watu kwenda kufanya uhalifu kwa vitu vya mtu, kuchoma vituo vya mafuta. Wale walioandamana ni wahalifu kama wahalifu wengine,” alisema Chifu Zakaria.

Kwa upande wake, Sheikh wa Msikiti wa BAKWATA Nyamwaga, Khalfan Shaban Mtongori, alisema “Mimi ninadhani ripoti ya tume itasaidia, inaweza kuwa chachu ya kuonya watu kwamba wakifanya vurugu watajulikana na kuchukuliwa hatua.”

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Mara, Joseph Nyiraha, alisema “Nilifuatilia ile ripoti na vipengele vyake hadi mapendekezo yaliyotolewa, mimi naona imekaa vizuri.”

Hata hivyo, walisema ripoti hiyo itakuwa na maana kama mapendekezo yake yatatekelezwa kwa vitendo na kwa wakati ili kuepusha kujirudia kwa matukio ya vurugu, kulinda amani na utulivu kwa maendeleo ya jamii na taifa.

“Moja ya mapendekezo ya tume ni suala la katiba mpya ambalo ni muhimu sana, maana kitu kikichukua muda mrefu sana kinakuwa na mapungufu kutokana na baadhi ya mambo kubadilika na kupitwa na wakati,” alisema Makabe.

"Utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya Tume utasaidia matukio haya yasijirudie tena. Watu wajitambue, wajielewe. Sisi shida yetu ni kuwa na amani hatutaki vurugu,” alisema Chifu Zakaria.

“Kama mapendekezo yaliyotolewa kwenye ile ripoti yatatekelezwa vizuri kwa busara na hekima, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia walioathiriwa na zile vurugu, amani na utulivu vitaendelea kudumu nchini,” alisema Nyiraha.

Viongozi hao walisisitiza kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya tume hiyo kwa ukamilifu utasaidia kuimarisha mifumo ya haki, uwajibikaji wa mamlaka husika na kukuza utamaduni wa uvumilivu wa kisiasa nchini.

Walieleza kuwa matukio ya uvunjifu wa amani si tu yanarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi, bali pia huacha majeraha ya kijamii yanayohitaji muda mrefu kupona.

Aidha, walipendekeza kuimarishwa kwa majukwaa ya majadiliano ya kitaifa na kijamii yatakayowezesha wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru, sambamba na elimu ya uraia kupewa kipaumbele ili kujenga uelewa sahihi wa haki na wajibu wa kila mmoja katika masuala ya kidemokrasia.

“Kama nilivyosema, ile ripoti iko vizuri, labda changamoto iwe kwenye utekelezaji wa mapendekezo. Na ningetamani kuona ile tume inakuwa ya kuhamasisha amani na kuelimisha vijana kuhusu umuhimu wa kulinda amani, itasaidia sana kuepusha yaliyotokea yasitokee tena,” alisema Sheikh Mtongori.

Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Uchunguzi, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, aliwasilisha ripoti ya uchunguzi huo kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, Aprili 23, 2026.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages