NEWS

Wednesday, 3 June 2026

Mbunge Mahera: Jimbo la Butiama linakwenda kunufaika bajeti mpya za afya, elimu, barabara



Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Wilson Mahera Charles, akizungumza Bungeni

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
------------------

Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Dkt. Wilson Mahera Charles, amesema wananchi wa jimbo hilo wana kila sababu ya kukaa mkao wa kufurahi, kwani wanakwenda kunufaika na bajeti mpya za kisekta za mwaka wa fedha 2026/2027.

Dkt. Mahera ametoa kauli hiyo leo Juni 3, 2026 katika mahojiano na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Bunge, jijini Dodoma, akitaja sekta zitakazonufaika zaidi kuwa ni afya, elimu na barabara, miongoni mwa nyingine.

“Kwenye sekta ya afya, Wizara ya Afya na ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI inayoshughulikia masuala ya afya ngazi ya msingi, naona wilaya ya Butiama tunakwenda kunufaika.

“Kwa mfano, hospitali yetu ya wilaya inakwenda kupata shilingi milioni 500 kutoka Serikali Kuu - ambazo zitakwenda kuongeza majengo,” amesema Mbunge Mahera.

Aidha, amesema shilingi milioni 300 zitapatikana kwa ajili ya kukamilisha vituo vya afya viwili; kimoja katika kata ya Butuguri na kingine kata ya Buhemba.

“Lakini pia, tumepata shilingi milioni 80 kwa ajili ya zahanati ya kijiji cha Nyanza kata ya Busegwe, na tumepata tena milioni 80 kwa ajili ya zahanati ya Nyakiswa kata ya Kianyari,” ameongeza.

Aidha, Dkt. Mahera amesema kwamba kupitia Mpango wa Uwekezaji wa Huduma ya Mama na Mtoto Tanzania (TMCHIP), Butiama imepata shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya Kirumi.

“Tunakwenda kuongeza miundombinu ya utoaji wa huduma za afya, hasa afya ya msingi katika wilaya ya Butiama. Kwa hiyo, yote hayo ni mafabikio makubwa sana na mambo mengine yanakuja,” amesema.

Kwa upande wa elimu, mbunge huyo amesema napo mambo mazuri yanakwenda kufanyika, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwenye chuo cha VETA Butiama.

“Pia, tumeomba kwamba ikitokea fursa ya nyongeza tupate shilingi milioni 386 kwa ajili ya ukamilishaji wa shule yetu ya amali pale Butasya, Butiama,” amesema.

Kwenye sekta ya barabara, Dkt. Mahera amesema “Tunashukuru kwamba kwenye bajeti hii [jimbo la Butiama] tumetengewa shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe na madaraja mbalimbali.”

Katika sekta ya barabara, amesema wamejipanga kuhakikisha pamoja na maeneo mengine, barabara ya Nyankanga-Rung’abure kwenda wilayani Serengeti yenye urefu wa kilomita 91 inajengwa kwa kiwango cha lami.

“Barabara hii imefanyiwa upembuzi yakinifu, kwa hiyo sasa hivi tunafanya jitihada kuhakikisha kwamba angalau inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kuelekea Serengeti.

“Lakini barabara yetu muhimu ya kiuchumi ya Busegwe kwenda Kitaramanka ya kilomita 38, nimeiongelea hapa [Bungeni] karibu mara nne - mara tano, na kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, nadhani kwenye bajeti ya mwaka mpya ijayo tutaanza upembuzi yakinifu ili kuhakikisha nayo inapitika kwa kiwango cha lami.

“Tukija Wizara ya Maji, kuna neema kubwa sana, napenda niwambie wananchi wa Butiama wakae mkao wa kufurahi, tunakwenda kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama ya bomba kutoka Ziwa Victoria katika vijiji mbalimbali vya jimbo letu la Butiama," amesema Dkt. Mahera.

Kuhusu vikundi vya wajasiriamali, hasa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, amesema vitaendelea kupata mikopo kutoka serikalini kwa ajili ya kuboresha makundi hayo kiuchumi na kijamii.

“Kwa hiyo, ukiangalia haya ni mafanikio makubwa sana, hivi vyote vinakwenda kuleta hali nzuri ya maisha katika jimbo letu la Butiama,” amesisitiza mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages