NEWS

Thursday, 4 June 2026

Waziri Aweso afanya mabadiliko ya wakurugenzi, mameneja sekta ya maji



Waziri Jumaa Hamidu Aweso

Na Christopher Gamaina
Mara Online News

Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumaa Hamidu Aweso, amefanya mabadiliko ya uongozi katika sekta ya maji kwa kuwabadilishia vituo vya kazi baadhi ya wakurugenzi na mameneja pamoja na kuteua wapya.

Taarifa iliyotolewea na wizara hiyo Juni 2, 2026 na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitendo cha Mawasiliano Serikalini, Florance Temba, ilieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha utendaji na kuboresha usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi nchini.

Mabadiliko yaliyofanyika ni ya wakurugenzi wasaidizi wizarani wawili, wakuu wa maabara wawili, mabadiliko ya kituo cha kazi kwa mameneja wa mikoa wa RUWASA 10 na wakurugenzi 15 wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira.

Aidha, Waziri Aweso amefanya uteuzi wa wakuu wa maabara za maji wawili, mameneja wa mikoa wa RUWASA watatu na wakurugenzi watendaji sita wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira

Mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati wa kuendelea kuimarisha utendaji ndani ya sekta ya maji ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuwafikishia wananchi huduma bora na endelevu ya maji yanafikiwa kwa wakati.

Hatua hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya maji mijini na vijijini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kiwango kinachokidhi mahitaji yao.

Miongoni mwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira waliobadilishiwa vituo vya kazi ni Esther Enock Gilyoma kutoka BUWSSA kwenda MUWASA mkoani Mara na Nicas Gervas Mugisha kutoka MUWASA kwenda Kasulu mkoani Kigoma.

Wakurugenzi na mameneja walioteuliwa na waliobadilishiwa vituo vya kazi wanatarajiwa kutumia uzoefu na weledi wao kusimamia kwa ufanisi rasilimali zilizopo, kuongeza mapato ya taasisi zao na kuhakikisha kuwa miradi ya maji inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.

Wadau wa sekta ya maji wameeleza kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuleta chachu mpya katika utendaji wa taasisi husika, hususan katika kipindi ambacho Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika upanuzi wa miundombinu ya maji nchini.

Mabadiliko hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha sekta ya maji kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku ikisisitiza uwajibikaji, ubunifu na matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages