NEWS

Wednesday, 3 June 2026

Rais Samia ndani ya Urusi kwa ziara ya kihistoria



Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania aliwasili nchini Urusi jana kwa ziara ya kitaifa kwa mwaliko wa Rais Vladimir Putin.

Na Mwandiishi Wetu

Rais wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa Rais wa pili wa Tanzania kufanya ziara ya kitaifa nchini Urusi, kuanzia leo Juni 3 hadi 5, 2026.

Ziara ya kwanza ya kiongozi wa Tanzania kutembelea taifa hilo kubwa barani Ulaya, ilifanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1969.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa Rais Samia anafanya ziara hiyo kwa mwaliko wa Rais Vladimir Putin wa Urusi, ambapo pia atashiriki na kuhutubia Jukwaa la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petetsburg (SPIEF 2026).

Jukwaa hilo ni miongoni mwa majukwaa makubwa yenye ushawishi duniani kwa mijadala ya uchumi, biashara na uwekezaji.

Jukwaa la SPIEF 2026, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, litakuwa ni fursa muhimu kwa Tanzania kuwasilisha ajenda yake ya uchumi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Tanzania na Urusi zina ushirikiano wa muda mrefu wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi tangu uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961.

Taarifa ya Ikulu ilieleza kwamba Rais Samia atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Putin, yatakayogusa uimarishaji wa sekta za kimkakati - biashara na uwekezaji, nishati, elimu, sayansi na teknolojia, madini, kilimo, miudombinu na utalii.

Taarifa ya Ikulu pia ilisema Rais Samia atashiriki katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi, litakalowakutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji na taasisi za kukuza biashara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages