
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.
Serengeti
----------------
Wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na mapori ya akiba Ikorongo- Grumeti na Jumuiya ya Uhifadhi ya Wanyamapori ya Ikona (WMA) wilayani Serengeti, wameomba kujengewa uzio kwa ajili ya kuzuia wanyamapori kuingia na kufanya uharibifu vijijini.
Waliwasilisha ombi hilo kwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alipofanya ziara katika wilaya hiyo na kusikiliza malalamiko ya wananchi hao kupitia mikutano ya hadhara, wiki iliyopita.
Wanavijiji hao walimwomba Kanali Mtambi awasaidie kuweka msukumo ujenzi wa uzio huo uharakishwe ili kuwaondolea madhila wanayopitia kutokana na uharibifu wa mazao kwenye mashamba yao unaofanywa na tembo, hali ambayo inawarudisha nyuma kimaendeleo.
Kanali Mtambi alikubali ombi hilo na hivyo kutumia nafasi hiyo kuagiza taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uzio huo.
“Wote tunakubali kuwa kuna athari za wanyamapori, lakini pia wote tunakubali kuwa kweli fence (uzio) itasaidia. Kwa vijiji ambavyo havina changamoto ya wapi fence ipite ujenzi wa uzio uanze mara moja,” Mkuu wa Mkoa aliagiza mbele ya wananchi na mamlaka zinazohusika na uwekeji wa uzio huo.
Hata hivyo, Kanali Mtambi alisema kwamba kwa vijiji vichache ambavyo havijakubaliana eneo ambalo uzio huo utapita vikae ili kutafuta suluhu ya pamoja, huku akiahidi kushirikiana navyo kufikia maamuzi mazuri.
Kwa upande wao, wananchi wa vijiji husika walisisitiza umuhimu wa kutekeleza agizo la ujenzi wa uzio huo haraka iwezekanvyo wakiamini utabadilisha hali ya maisha yao.
“Sisi tunahitaji fence kwa haraka zaidi badala ya kuendelea kucheleweshwa,” alisema mmoja wa wakazi wa vijiji hivyo.
Walilamika pia kwamba mbali na kuharibu mashamba yao ya mazao ya chakula na biashara, wanyamapori wanaovamia vijiji vyao, wakiwemo tembo, samba na chui wamekuwa wakitishia usalama wa maisha yao mara kwa mara.

Tembo
“Zaidi ya watu sita wamejuruhiwa na simba kwa mwaka huu tu, na tembo ni wengi, kila wakati wanaharibu mashamba,” alilalamika mwananchi mwingine.
Wananchi hao walisema mikutano yote ya vijiji imeshapitisha mpango huo wa uwekaji wa uzio huo, hivyo wanashangaa kwanini utekelezaji wake unaendelea kuchelewa.
Kampuni ya Grumeti Fund ambayo inasaidia uhifadhi wa wanyamapori na maendeleo ya jamii katika vijiji hivyo iko tayari kufadhili mradi wa ujenzi wa uzio huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake katika kupunguza migongano ya binadamu na wanyamapori.
Baadhi ya vijiji ambavyo vipo kwenye orodha ya kunufaika na mpango huo ni Park Nyigoti, Makundusi, Nyichoka, Natta-Mbiso na Bokore.
Maisha ya maelfu ya wakazi wa vijiji hivyo hutegemea kilimo na ufugaji kuendesha maisha yao licha ya kukabiliwa na uvamizi wa tembo kwa miaka mingi.
Wahifadhi kutoka serikalini pia wanakiri kuwa ujenzi wa uzio wa umeme kutenganisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori, mashamba na makazi ya wananchi utakuwa suluhisho la madhara yanayosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment