
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara, Ayub Mwita Makuruma (aliyevaa kaunda suti nyeusi), akiongoza wajumbe wa jumuiya hiyo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Serengeti jana.
Serengeti
----------------
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Mara imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Jumuiya hiyo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Ayubu Mwita Makuruma, ilieleza hayo jana Alhamisi baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali.
Makuruma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, alisema wao kama ALAT Mkoa wa Mara wameridhishwa na utekelezwaji wa miradi waliyoitembelea.

Makuruma akiongoza wajumbe wa ALAT kukagua miradi
Hata hivyo, jumuiya hiyo ilielekeza utekelezaji miradi hiyo uharakishwe kwa kuzingatia michoro ya ramani na viwango vya ubora ili kuwaletea wananchi maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Miongoni mwa miradi hiyo ni jengo la kituo cha afya Sedeko linaloendelea kujengwa kwa gharama ya shilingi milioni 269.5, kati ya hizo, milioni 250 ni kutoka Serikali Kuu na milioni 19.5 ni michango ya wananchi.
Katika ziara hiyo, ALAT Mkoa wa Mara ilielezwa kuwa shilingi milioni 250 nyingine zimetengwa kwa ajili ya jengo la wazazi kituoni hapo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mradi mwingine uliotembelewa ni ujenzi wa jengo la ofisi ya kata ya Morotonga utakaogharimu shilingi milioni 85.76 kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, huku michango ya wananchi ikiwa shilingi milioni 13.6.
Nalo jengo la utawala la halmashauri hiyo linajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 42.
Kutokana na kufurahishwa na utekelezaji wa mradi wa ofisi ya kata ya Morotonga, ALAT Mkoa wa Mara iliamua kuizawadia kata shilingi milioni moja kwa ajili ya kununua samani.

Makuruma akikabidhi fedha hizo
"Nitoe pongezi kwa mradi huu, hongereeni sana... kama mmechora ramani wenyewe basi TAMISEMI wajifunze kwenu, mradi unaridhisha,” alisema Mjumbe wa ALAT Mara, George Machera Nyamaha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
"Huu ni miongoni mwa miradi itakayoipa heshima Serengeti wakati wa mbio za Mwenge mwezi ujao," alisema Diwani wa Kata ya Morotonga, Musa Magasi.
No comments:
Post a Comment