NEWS

Saturday, 1 August 2026

Mara wapokea Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, kukagua miradi ya mabilioni ya shilingi



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia), akipokea hati ya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru 2026 kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringa Macha, mapema leo Jumamosi.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
---------------

Mwenge wa Uhuru 2026 umepokewa mkoani Mara mapema leo Jumamosi baada ya kuhitimisha mbio zake mkoani Simiyu jana Ijumaa.

Mapokezi yamefanyika katika Shule ya Msingi Balili wilayani Bunda, yakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringa Macha.

Jana, Kanali Mtambi waliwambia waandishi wa habari mjini Musoma kwamba mwenge huo utapita kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 63 yenye thamani ya shilingi bilioni 174.

Kati ya kiasi hicho cha fedha, milioni 145.4 ni kutoka Serikali Kuu, bilioni 14.8 (wahisani), bilioni 12.2 (nguvu kazi ya wananchi) na bilioni 2.2 (halmashauri za mkoa huo).

Alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika halmashauri zote tisa za mkoa wa Mara kwa umbali wa kilomita 966 kuanzia Agosti 1 hadi 9, 2026.

Halmashauri hizo ni Bunda TC, Bunda DC, Butiama DC, Musoma DC, Musoma MC, Rorya DC, Tarime TC, Tarime DC na Serengeti DC.

Pamoja na matukio mengine, ukiwa wilayani Butiama kesho Jumapili, Mwenge wa Uhuru utawasha Mwenge wa Mwitongo nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kanali Mtambi ametoa wito kwa wananchi wa Mara kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru na kushiriki katika matukio yake yaliopangwa kufanyika katika mkoa huo.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 ni “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages