NEWS

Thursday, 30 July 2026

Serikali, wawekezaji, watoa huduma migodini wajadili fursa sekta ya madini



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, azungumza katika kikao cha ‘Mining Breakfast Briefing jijini Dar es Salaam leo.

Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
---------------------

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya madini kupitia majukwaa ya majadiliano ili kujenga sekta yenye ushindani, inayovutia uwekezaji na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mavunde ameyasema hayo katika kikao cha ‘Mining Breakfast Briefing (MBB)’, kilichoandaliwa kwa ushirikiano wa Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) na Wizara ya Madini, ambapo ametoa wito kwa wadau kuendelea kutumia majukwaa hayo kujadili fursa na changamoto zinazohusu sekta ya madini.

Amewashukuru viongozi na wanachama wa TCM kwa kuendelea kutoa nafasi kwa serikali na wadau kukutana na kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya sekta hiyo, huku akiipongeza Mantra Tanzania Limited kwa kudhamini kikao hicho.

Waziri Mavunde amesema ushiriki wa wadau katika majukwaa hayo unaonesha dhamira ya pamoja ya kujenga sekta ya madini yenye ushindani, inayovutia mitaji na teknolojia, pamoja na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kikamilifu kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Serikali inathamini utaratibu huu wa kukutana na wadau wa sekta ya madini kupitia Mining Breakfast Briefing, kwa kuwa unatoa fursa ya kufanya mazungumzo yenye tija, kujenga uelewa wa pamoja, kupokea changamoto zinazojitokeza na kutafuta suluhisho kwa pamoja,” amesema.

Kwa mujibu wa Wazriri Mavunde, serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo katika kutatua changamoto zinazojitokeza na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuongeza uzalishaji, ajira na mapato ya serikali.

Hivyo, ametumia fursa hiyo pia kuwataka watoa huduma migodini kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodini.

“Ni vyema kuendelea kukutana mara kwa mara kupitia jukwaa hili muhimu, kwa sababu linatupa nafasi ya kusikilizana, kujadiliana na kutafuta suluhisho la changamoto zinazotukabili kwa pamoja,” amesema.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amewashukuru wadau wa sekta ya madini kwa kushiriki katika kikao hicho, akiwataka kuongeza ushirikiano na mshikamano katika kukuza sekta hiyo.

Mhandisi Samamba amesema ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kutatua changamoto, kuchochea uwekezaji na kuhakikisha fursa zinazotokana na rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa mapana ya taifa.

Amesisitiza kuwa mawasiliano ya mara kwa mara kati ya serikali na wadau yataendelea kuwa nyenzo muhimu katika kubaini changamoto mapema na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.

Mhandisi Yahaya Samamba akizungumza kwenye kikao hicho

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Philbert Rweyemamu, amemshukuru Waziri Mavunde kwa kuendelea kudumisha uhusiano mzuri na wadau wa sekta ya madini.

Mhandisi Rweyemamu amesema utaratibu wa serikali wa kukutana mara kwa mara na wadau kupitia Mining Breakfast Briefing ni muhimu katika kujenga mawasiliano ya karibu, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Amesema TCM itaendelea kushirikiana na serikali chini ya uongozi imara Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuimarika, kuvutia uwekezaji na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Akizungumzia maendeleo ya mradi wa uranium, Meneja wa Uendelevu wa Mantra Tanzania Limited, Majani Wambura, amesema umebaini uwepo wa hifadhi ya takriban tani 58,500 za uranium, huku uzalishaji ukitarajiwa kufikia tani 3,000 kwa mwaka.

Majani Wambura akizungumza katika kikao hicho

Wambura amesema mradi wa uranium unatarajiwa kutoa ajira kwa wafanyakazi zaidi ya 4,000 baada ya kuanza uzalishaji, hatua itakayochochea shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa meneja huyo, mradi huo unatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2029 na utakuwa na maisha ya miaka zaidi ya 20, huku utafiti ukiendelea ili kubaini uwepo wa rasilimali zaidi katika maeneo yanayohusishwa na mradi huo.

Hatua zote hizo zitaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa 10 wa uraniaum duniani.

Uranium ni rasilimali yenye matumizi mbalimbali, ikiwemo katika uzalishaji wa nishati ya umeme na sekta ya afya, hususan matumizi ya mionzi katika uchunguzi na matibabu.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, akizungumza katika kikao hicho.

Akifunga jukwaa hilo, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema serikali na wadau wa sekta ya madini wanapaswa kuendelea kukutana mara kwa mara kupitia MBB ili kujadili na kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Dkt. Kiruswa amesema mikutano ya mara kwa mara itasaidia kujenga mawasiliano na uelewa wa pamoja kati ya serikali na wadau, kujadili changamoto na fursa zilizopo, pamoja na kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages