
Ndege ya ATCL ikitua kwenye Uwanja wa Ndege Musoma mkoani Mara, Septemba 17, 2026.
Baada ya miaka minane ya kusitisha safari zake za anga katika mji wa Musoma mkoani Mara, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeanzisha safari hizo tena ili kuendeleza fursa lukuki za kiuchumi zinazopatikana katika eneo hilo la kanda ya Ziwa Victoria.
ATCL ilirejesha huduma zake za anga katika mji wa Musoma, ulioko kandokando ya Ziwa Victoria, Septemba 17, 2026.
Wananchi wengi wa mji wa Musoma, wakiwemo wafanyabiashara, walishangilia kwa nderemo na vifijo kurejea kwa huduma za anga za ATCL, ikiwa ni ishara ya kuashiria kufunguliwa upya kwa diridha la kiuchumi mkoani Mara.
Mkoa wa Mara, ambao wakati wa ukoloni wa Waingereza ulikuwa sehemu ya jimbo kubwa lililoitwa Lake Province likijumuisha mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza, Simiyu na Shinyanga, unasifika kwa shughuli za kilimo cha mazao ya biashara ya pamba na kahawa, uchimbaji wa madini ya dhahabu, uvuvi, ufugaji na utalii unaotokana na kuwepo kwa hifadhi bora Afrika – Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Inatarajiwa kwamba kuanza upya kwa safari za ndege za ATCL siyo tu kutachochea kasi ya ukuaji wa sekta hizo muhimu kwa uchumi wa Tanzania, bali pia itakuwa kivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao kwa kuangalia maendeleo ya kila sekta.
Kijiografia, Mara ni mkoa uliokaa kimkakati kwa kupakana na nchi jirani ya Kenya, eneo ambalo kuna mtiritiko wa ushirikiano wa kibiashara baina ya Watanzania na Wakenya tangu enzi za ukoloni.
Kurejea kwa safari za ndege za ATCL kufuatia upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Musoma, ni fursa kubwa kwa wananchi wa Mara kubuni shughuli mbalimbali zitakazowapatia kipato kwa kuzalisha bidhaa kwa wingi zitazohitajika maeneo mengine nje ya mkoa wao.
Maneno mazuri ya kuwahamasisha wananchi wa mkoa wa Mara yalitamkwa na Katibu Tawala wa mkoa huo, Gerald Kusaya, alipowataka kuchamngamkia fursa za kiuchumi ziletwazo na urejeo wa usafiri wa kuaminika wa ndege za ATCL.
Ndege za ATCL zinazofahamika kwa jina la Air Tanzania zitakuwa zikifanya safari zake Musoma siku za Alhamisi na Jumamosi, kwa mujibu wa ratiba ya shirika hilo.
"Hii fursa ya usafiri wa ATCL imetujia miguuni petu... labda tushindwe wenyewe," alisema mfanyabiashara Rhobi Chacha, mchuuzi wa samaki mjini Musoma.
No comments:
Post a Comment