NEWS

Thursday, 30 July 2026

Hope for Girls na Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji Tanzania



Sehemu ya mikutano ya Shirika la HGWT ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji

Na Mwandishi Wetu
Mara
-----------

Baada ya kupata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, sasa kipaumbele cha Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji 2025/26 – 2029/30 kwa kutoa elimu ya kupiga vita mila hiyo mkoani Mara.

Utekelezaji wa mkakati huo wa serikali unahusisha utoaji wa elimu ya madhara ya ukeketaji watoto wa kike na kuisisitiza jamii kuachana na ukatili huo wa kijinsia, kwani ni ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu.

Akizungumza katika utoaji wa elimu hiyo katika wilaya za Serengeti na Tarime wiki hii, Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly, alisema lengo ni kupunguza kiwango cha ukeketaji nchini kwa asilimia 50, kutoka asilimia nane mwaka 2024/25 hadi asilimia nne ifikapo 2029/30.

“Tunaamini ukeketaji utatokomezwa na wasichana ambao ndio wahanga wakubwa watakuwa salama na kuweza kusoma na kutimiza ndoto zao,” alisema Rhobi ambaye pia ni mjumbe wa timu inayosambaza mkakati huo kwa kushirikiana na maafisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly, akihamasisha kampeni ya utekelezaji wa mkakati huo wa serikali.

Katika kampeni hiyo ya utoaji elimu na usambazaji wa Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji 2025/26 – 2029/30, wadau mbalimbali waliipongeza HGWT kwa kuendeleleza mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, hususan ukeketaji na ndoa za utotoni katika mkoa wa Mara.

Kwamba HGWT imekuwa na mchango mkubwa katika kuijengea jamii uelewa wa madhara ya ukeketaji, kuokoa na kuwezesha wasichana wengi kutimiza ndoto zao katika mkoa wa Mara ambao umekuwa ukiripotiwa kuwa na vitendo vingi vya ukatilii wa kijinisia.

Mkazi wa wilayani Serengeti, Wankuru Marwa, alisema shirika hilo limekuwa mkombozi kwa wasichana wengi katika ambao ndoto zao zingefifia na kupotea.

“Wasichana ambao walikuwa katika hatari ya kukeketwa ili waozeshwe na wazazi wao, wameendelezwa kielimu. Uwepo wa shirika hili umekuwa msaada mkubwa. Naiomba Serikali ichukue hatua kali kwa wazazi wanaokiuka sheria na kutaka kuwakeketa watoto wao,” alisema Wankuru.

Boniphace Samson wa wilayani Serengeti pia alisema ushirikiano kati ya serikali, viongozi wa jadi na HGWT umesaidia wasichana wengi mkoani Mara kupata fursa sawa ya kusoma na kutimiza ndoto zao bila hofu ya ukatili.

Rhoda Chacha wa wilayani Tarime alisema HGWT imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwelewa kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara na makongamano mbalimbali vijijini.

Mkazi wa kata ya Itiryo wilayani Tarime Anitha Nyangi, ambaye zamani alikuwa ngariba (mkeketaji), alisema "Nilielimishwa madhara ya ukeketaji, nikaambiwa ni kosa kisheria, nikaacha. Kwa sasa mimi ni balozi wa kuelimisha wananchi wasikekete watoto wa kike, bali wawasomeshe kwa faida yao siku za usoni.”

Nyangi aliongeza: “Nilikuwa nataka kumkeketa binti yangu ili aolewe lakini alikimbia na kwenda nyumba salama Hope for Girls. Leo hii anasoma chuo kikuu mwaka wa tatu, anasoma uhasibu. Nina imani atatimiza ndoto zake ambazo nilitaka kuzikwamisha.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alitumia fursa hiyo kulishukuru Shirika la HGWT kwa jitihada inazofanya kupinga ukeketaji na kuhamasisha maendeleo na ustawi wa watoto wa kike.

“Katika kampeni hii tumejifunza kuwa ukeketaji si utamaduni unaostahili kuendelezwa, bali ni ukatili wa kijinsia, ukiukwaji wa sheria na haki za binadam. Natoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, mil ana jamii tushirikiane kupinga mila hii,” alisema Meja Gowele.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto), akikabidhiwa kitabu cha mkakati huo.

Naye Katibu wa Mila Taifa, Chifu Girihuida Shumbu, alisema mtoto wa kike ana haki ya kuishi salama, kuthaminiwa, kupata elimu ili kutimiza ndoto zake, hivyo wataendelea kuhamasisha jamii kulinda haki hizo.

“Kwa umoja wetu na kwa niaba ya wazee wa mila, nasema ukeketaji ni kinyume cha sheria na haki za binadamu,” alisema Chifu Shumbu.

Kwa upande wake Mhamasishaji kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Suleman Bishagazi, alisema mkakati huo umewashirikisha wadau wote na kuwapa nafasi ya kuwajibika kuhakikisha ukeketaji unatokomezwa nchini.

Bishagazi alisisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda mtoto wa kike na mwanamke dhidi ya ukeketaji na kwamba serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kuhamasisha mila hiyo.

HGWT yaokoa maelfu ya wasichana
Taarifa zilizopo zinaonesha Shirika la HGWT limeokoa wasichana 4,481 waliokuwa katika hatari ya kukeketwa kwa nguvu mkoani Mara kati ya mwaka 2017 na 2025.

Wasichana hao walipata hifadhi katika nyumba salama ambazo zinamilikiwa na kuendeshwa na HGWT katika wilaya za Serengeti na Butiama.

Wakiwa katika nyumba salama hizo, walipata huduma mbalimbali kama vile msaada wa kisaikolojia, huduma za kiafya, kuendelezwa kielimu na msaada wa kisheria.

Baadhi ya wasichana hao tayari wamehitimu vyuo vikuu, vyuo vya kati, ufundi, elimu ya sekondari na msingi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly, mafanikio hayo yamechangiwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanaolipa shirika hilo ushirikiano wa hali na mali.

Wadau hao ni pamoja na Tanzania Development Trust-UK Charity, Netzwerk Rafael- Germany, Polish Aid, Kiabakari Foundation na Hope for Girls and Women- France, French Embassy- Tanzania na FAWCO Foundation.

Wengine ni Grumeti Reserves, Mapito Camp, Four Seasons Hotels, Nomad Tanzania, June Powell, UNFPA/C-Sema, ACP- France, Wojiciech Adam, Koscielniak, Julian na Ann Marcus.

Umuhimu wa Mkakati wa Kutokomeza Ukeketaji
Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji 2025/26 - 2029/30 unalenga kuunganisha juhudi za sekta mbalimbali ili kutokomeza ukeketaji na kulinda haki, afya na ustawi wa wanawake na watoto wa kike nchini.

Mkakati huo wa serikali unasisitiza kuwa ukeketaji ni ukiukwaji wa haki za binadamu na unalenga kuhakikisha kila mtoto wa kike analindwa dhidi ya ukatili huo na anaishi katika mazingira salama.

Unahamasisha utoaji wa elimu kwa jamii ili kubadili mitazamo inayounga mkono ukeketaji, kwa kuzingatia mazingira ya kitamaduni na kushirikisha viongozi wa kimila na kidini katika kuleta mabadiliko ya tabia.

Vilevile, mkakati huo unasisitiza utekelezaji wa sheria zilizopo na kuimarisha mifumo ya kisera ili kuzuia ukeketaji, kuwawajibisha wahusika na kutoa ulinzi kwa watoto walio katika hatari.

Lakini pia, unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi kwa manusura wa ukeketaji, ikiwemo huduma za afya, ushauri wa kisaikolojia, msaada wa kisheria na huduma za ustawi wa jamii.

Lengo kuu la serikali ni kupunguza kiwango cha ukeketaji nchini kutoka asilimia nane hadi asilimia nne ifikapo mwaka 2030, kupitia ushirikiano wa serikali, jamii na wadau wa maendeleo.

Dhamira kuu ya serikali ni kupungua ukeketaji na skuboresha huduma za afya, elimu na usawa wa kijinsia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan lengo la kutokomeza vitendo vyenye madhara dhidi ya wanawake na watoto wa kike ifikapo mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages