
Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Esther Gilyoma, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake mjini Musoma.
Musoma
----------------
Huduma ya maji ya bomba imeimarika kwa wakazi wa manispaa ya Musoma mkoani Mara, kufuatia kukamilika kwa utatuzi wa hitilafu ya mtambo wa kusukuma maji katika eneo la Bukanga.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), hitilafu ya mtambo huo ilisababisha wananchi hao, hasa wanaoishi kwenye miinuko kukabiliwa na upungufu wa maji kwa zaidi ya mwezi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Alhamisi, Septemba 24, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Esther Gilyoma, aliomba radhi wananchi kutokana na usumbufu uliojitokeza, akisema tatizo hilo lilikuwa nje ya uwezo wa mamlaka hiyo.
“Tumepitia changamoto kubwa kwa zaidi ya mwezi na malalamiko ya wananchi yalikuwa mengi, lakini hili lilikuwa nje ya uwezo wetu,” alisema Gilyoma.
Alisema hali hiyo iliilazimu MUWASA kufanya mgawo wa maji kwa wateja wake wakati hatua za kuimarisha huduma hiyo zikiendelea.
“Wale waliokuwa wanapata maji waliendelea kupata kwa maeneo ambayo hayakuathiriwa, lakini kwa wale ambao wako maeneo ya miinuko walikumbwa na kadhia hii.
“Niwaombe radhi wakazi wa manispaa ya Musoma pamoja na maeneo jirani yanayohudumiwa na MUWASA, hatukufanya makusudi bali ilikuwa nje ya uwezo wetu,” alisisitiza Gilyoma.
Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Wizara ya Maji iliingilia kati na kuwezesha upatikanaji wa kifaa kutoka Mamlaka ya Maji Same-Mwanga, ambacho kilifungwa na kuanza kusambaza huduma.
Aidha, alisema kifaa ambacho MUWASA kupitia Wizara ya Maji ilikiagiza kutoka nchini China tayari kimeshaletwa kwa ajili ya kufanyiwa majaribio.
Gilyoma alisema hatua hiyo sehemu ya jitihada za haraka za kuhakikisha huduma ya maji inarejea katika hali ya kawaida kwenye maeneo yote yaliyoathirika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MUWASA, kuimarika kwa huduma hiyo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya uzalishaji wa maji eneo la Bukanga.
“Wizara ya Maji imeweka shilingi zaidi ya bilioni 30, ni uwekezaji mkubwa. Hakuna mradi au miundombinu ya maji inayoweza kufanyika pasipokuwa na rasilimali fedha,” alisema.
Gilyoma alisema uwekezaji huo utawezesha huduma ya maji kuwa endelevu katika manispaa ya Musoma na maeneo mengine yanayohudumiwa na MUWASA.
Hivyo, alisisitiza kuwa mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na uhakika wa kupata huduma ya maji ambayo ni msingi wa afya, usafi na shughuli za kila siku.
“MUWASA tumejipanga kuwahudumia wananchi na niwahakikishie huduma ya maji siyo ya leo tu bali ni endelevu. Maji ni uhai na hayana maskini wala tajiri,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MUWASA alitumia nafasi hiyo pia kuishukuru Wizara ya Maji kwa namna ilivyosaidia katika kutatua changamoto iliyokuwepo.
Alisema maelekezo na msaada uliotolewa na viongozi wa wizara hiyo uliwezesha MUWASA kuchukua hatua za haraka katika kurejesha huduma kwenye maeneo yaliyoathirika.
“Kipekee napenda kumshukuru Mungu tumepitia changamoto lakini ametuvusha. Wizara ya Maji imetupa maelekezo na imetusaidia kupitia viongozi wetu - Waziri wa Maji na Katibu Mkuu.
“Lakini tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ametuwezesha kuweka mitambo ya uzalishaji wa maji katika eneo letu la Bukanga,” alisema Gilyoma.
Wajipanga kukabiliana na El Niño
Katika hatua nyingine, Gilyoma alisema MUWASA imeanza maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño.
Alisema mamlaka hiyo tayari imepokea maelekezo kutoka Wizara ya Maji na imeunda timu maalum kwa ajili ya kuhakikisha huduma kwa wananchi inaendelea kutolewa katika mazingira yoyote.
MUWASA ni moja ya mamlaka za maji nchini ambazo zimefanikiwa kuvuka lengo la Ilani ya CCM la kufikia asilimia 95 ya wananchi wanaopata majisafi mijini kufikia 2025, ambapo imefikia asilimia 98 ya wanaopata huduma hiyo katika manispaa ya Musoma.
Mbali na manispaa ya Musoma, MUWASA pia inasambaza huduma ya majisafi kwa wakazi wa miji ya Shirati wilayani Rorya, Mugumu wilayani Serengeti na Tarime.
No comments:
Post a Comment