
Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa, akiwa kwenye Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam
--------------------
Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, amewaagiza wafanyakazi wa shirika hilo la umma kufanya kila liwezekanalo kutunza Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam ili iendelee kuwa kivutio cha watalii wa ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Kamishna Mwishawa, ni wajibu wa TANAPA kutunza malikale zote nchini ili kuhifadhi historia ya taifa na kukuza pato kiuchumi.
Nyumba hiyo ndipo alipoishi gwiji huyo wa siasa barani Afrika wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.
Baada ya kupatikana uhuru Desemba 9, 1961, Mwalimu Nyerere alihamia Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.
Kamishna Mwishawa alitoa wito wa kutunza nyumba hiyo jijini Dar es Salaam juzi, alipofanya ziara ya kikazi na mazungumzo na maafisa na askari uhifadhi wa Ofisi Kiunganishi TANAPA.
Kiongozi huyo alipata fursa ya kukagua mradi wa ukarabati wa zahanati ya Ilala Bungoni unaotekelezwa na Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya TANAPA (TIL).
Mradi huo unahusu ukarabati wa ofisi ya idara ya afya ya jiji la Dar es Salaam, kituo cha afya Buguruni na zahanati ya Bungoni.
Kamishna Mwishawa aliwapongeza wasimamizi wa miradi hiyo ya ukarabati.

Katika ziara hiyo, Kamishna Mwishawa alifuatana na viongozi mbalimbali wa TANAPA na Mtendaji Mkuu wa TIL.
No comments:
Post a Comment