NEWS

Tuesday, 22 September 2026

Rorya: Moto bweni la Prof. Sarungi Sekondari umesababisha hasara ya mali za milioni 85.9/-




Na Christopher Gamaina

Ajali ya moto ulioteketeza bweni la wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Prof. Sarungi iliyopo wilaya ya Rorya mkoani Mara, imesababisha hasara ya mali zenye thamani ya shilingi milioni 85.9.

Kati ya hizo, milioni 66.77 ni thamani ya jengo hilo na samani zake, huku milioni 19.13 ikiwa thamani ya mali mbalimbali za wanafunzi 80 waliokuwa wanatumia bweni hilo.

“Hiyo ni kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika baada ya ajali hiyo ya moto,” Makamu Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Benard Okombo, aliiambia Mara Online News kwa njia ya simu jana Jumatatu.

Mwl. Okombo alisema ajali hiyo iliotokea Septemba 16, 2026 saa tatu usiku wakati wanafunzi wote 80 na wengine wa shule hiyo wakiwa kwenye vipindi vya masomo madarasani.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, chanzo cha moto huo kinadaiwa kuwa hitilafu ya umeme (short circuit) iliyotokea baada ya umeme kukatika na kurejea ghafla.

“Kwa bahati, hakuna mwanafunzi wala mwalimu aliyejeruhiwa,” alisema Makamu Mkuu huyo wa shule.

Isipokuwa wanafunzi 80 waliokuwa wakitumia bweni hilo wameathirika kwa kupoteza vifaa na mali mbalimbali, hali ambayo imeongeza changamoto kwa shule hiyo.

Jambo la faraja ni kwamba wadau mbalimbali wamejitokeza kutoa misaada ya kuwasaidia wanafunzi waliopoteza sehemu kubwa ya mahitaji yao kuendelea na maisha ya shule.

Misaada iliyolewa hadi sasa, kwa mujibu wa Mwl. Okombo, inajumuisha magodoro 80, sabuni ya unga pakti 163, miche 196 ya sabuni za kufulia, miswaki 89, dawa ya meno pakti 84, counter books 300, mafuta ya kujipaka kopo 148, vyandarua 80 na sahani 97.

Hata hivyo, shule hiyo bado inahitaji misaada zaidi, ikiwemo gharama za kukarabati au kurejesha jengo la bweni lililoungua na vifaa muhimu vya wanafunzi walioathirika.

Hivyo, Diwani wa Kata ya Nyahongo ilipo Shule ya Sekondari Prof. Sarungi, Samson Kagutu, ametoa wito kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wazazi, wafanyabiashara na taasisi kujitokeza kutoa michango itakayosaidia kuirejea katika hali yake ya kawaida.

Kagutu alisema michango hiyo ni muhimu zaidi, hasa kipindi hiki cha kuelekea mitihani ya kitaifa, ambapo wanafunzi wanahitaji mazingira salama na tulivu ili kujiandaa kikamilifu.

Alibainisha kuwa Shule ya Sekondari Prof. Sarungi yenye wanafunzi 1,346 (wavulana 731 na wasichana 615) ni miongoni mwa shule za sekondari zinazotegemewa wilayani Rorya kwa matokeo bora ya mitihani ya kitaifa.

“Tunaomba wazazi na wadau wengine wajitokeze kutusaidia kwa chochote turudhishe hadhi ya shule hii kuelekea kwenye mitihani ya kitaifa ili wanafunzi waweze kufanya mitihani kwa amani.

“Prof Sarungi ni moja ya shule za sekondari katika wilaya ya Rorya zinazotegemewa kwa matokeo mazuri, mara nyingi imekuwa ikiongoza kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne,” alisema Diwani Kagutu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages