NEWS

Monday, 3 August 2026

Mwenge wa Uhuru wawasha Mwenge wa Mwintongo kumuenzi Mwalimu Nyerere



Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang'onda, akitumia Mwenge wa Uhuru kuwasha Mwenge wa Mwitongo nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika wilaya ya Butiama, mkoani Mara jana.

Na Mwandishi Wetu
---------------------------
Kuwashwa kwa Mwenge wa Mwintongo nyumbani kwa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, litakuwa ni tukio kubwa nchini Tanzania kwa miaka mingi ijayo kama kumbukumbu ya kumuenzi kiongozi huyo shujaa aliyepigania uhuru na amani siyo tu katika taifa lake, bali bara zima la Afrika.

Mwenge wa Mwintongo, mahali alipozaliwa Mwalimu Nyerere katika wilaya ya Butiama, mkoani Mara, uliwashwa juzi katika mbio za kitaifa za Mwenge wa Uhuru zinazoendelea.

Ni tukio kubwa lililovuta hisia za wakazi wa Butiama kwa kumuenzi mwananchi mwenzao shupavu aliyekuwa mstari wa mbele kujitoa mhanga na kuwakabili wakoloni uso-kwa-uso akidai waliachie koloni la Tanganyika liwe huru.

Mwalimu Nyerere ndiye aliyebuni Mwenge wa Uhuru kuwa alama ya taifa inayoonesha uhuru, matumaini, amani na umoja kwa Watanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia) katika picha ya pamoja na viongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Mwitongo nyumbani kwa Mwalimu Nyerere.

Ni alama hiyo hiyo iliyowekwa Butiama kwa Mwenge wa Mwintongo ili kuendelea kuleta matumaini ya amani na umoja kwa Watanzania, ikiwa ni kumbukumbu ya tunu za amani na haki kwa watu wote - zilizoachwa na Mwalimu Nyerere kwa Tanzania, Afrika na dunia.

Mwenge wa Uhuru, ambao leo umeingia siku ya tatu ya kukimbizwa mkoani Mara, uliwashwa kwa mara ya kwanza kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanganyika. Kazi hiyo ilifanywa na Alexander Nyirenda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, ambalo zamani chini ya wakoloni Waingereza lilijulikana King's African Rifles (KAR).
Ukiwa unakimbikizwa mkoani Mara, mwenge huo umepangwa kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 63 yenye thamani ya shilingi bilioni 174.

Mwenge huo, ambao utakimbizwa katika halmashauri zote tisa za mkoa wa Mara, uliingia mkoani Mara Agosti 1, mwaka huu ukitokea mkoa wa Simiyu.

Makabidhiano ya mwenge huo yalifanyika katika Shule ya Msingi Balili wilayani Bunda kati ya wakuu wa mikoa, Kanali Evans Mtambi wa Mara na Anamringi Macha wa Simiyu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages