NEWS

Tuesday, 4 August 2026

Miradi ya CSR Barrick yang'ara Mbio za Mwenge wa Uhuru Tarime Vijijini



Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda (kulia aliyevaa skafu), wakati wa uzinduzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Matongo wilayani Tarime jana. Mwingine aliyevaa skafu ni Mkuu wa wilaya hiyo, Meja Edward Gowele.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-----------

Mbio za Mwenge wa Uhuru wa Uhuru Kitaifa 2026, jana zilizindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi iliyotekelezwa na Mgodi wa Dhadabu wa North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Mradi hiyo ni vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa katika Shule ya Sekondari Matongo inayohudumia mamia ya wanafunzi kutoka maeneo ya jirani na mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mradi huo umetekelezwa na mkandarasi mzawa kwa gharama ya shilingi milioni 63.8 ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi.

Mradi mwingine ni ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Kituo cha Afya Magoto kilichopo kata ya Nyakonga, ambao pia unatekelezwa na mkandarasi mzawa kwa gharama ya shilingi milioni 229.7 kupitia CSR Barrick North Mara.

Akizungunza mara baada ya kukagua na kuzindua mradi huo wa vyumba viwili vya madarasa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, aliipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuunga mkono juhudu za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Mwang’onda alisema ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo unaendelea kuzaa matunda chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka mazingira mazuri ya uwekezaji yanayowezesha sekta binafsi kushiriki katika kuchochea maendeleo ya wananchi.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mwang'onda, akizungumza katika hafula hiyo.

“Namshukuru Rais Samia kwa jinsi ambavyo anajenga mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo, kwani hapa tunashuhudia wadau wetu wa maendeleo, Barrick, wakifanya kazi kubwa kwa kushirikiana na serikali,” alisema.

Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alisema fedha zilizowezesha ujenzi wa madarasa hayo ni sehemu ya mapato ambayo Barrick inairejesha kwa jamii kutokana na shughuli zake za uchimbaji madini nchini.

“Barrick wametoa fedha ambayo wanarudisha kwa serikali kutokana na shughuli wanazofanya katika nchi yetu. Tunawashukuru sana kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya, tumeambiwa hapa pia kuna jengo la utawala na maabara, wamefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na serikali.

“Namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluu Hassan kwa jinsi anavyoendelea kuboresha setka ya elimu nchini. Hata wanafunzi wetu hawa wanasoma bure kuanzia elumu ya msingi,” alisema Mwang’onda.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Matongo wakishuhudia uzinduzi wa vyumba hivyo vya madarasa katika shule yao

Akihitimisha azungumzo yake kwenye mradi huo wa elimu, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alisema Mwenge wa Uhuru umevutiwa na ubora wa mradi huo na kuridhishwa na namna ulivyotekelezwa.

“Niseme tu kwamba Mwenge wa Uhuru umefurahishwa sana na ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa na uko tayari kuvizindua,” alisema Mwang’onda na kupigiwa makofi na mamia ya wananchi waliojitokeza kuhuhudia tukio hilo.
Ukaguzi wa miradi

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zablon Obuya Orege, mradi huo ulianza kutekelezwa Juni 21, 2025 na kukamilika Juni 29, 2026.

“Hadi sasa mkandarasi aliyetekeleza mradi huu amelipwa kiasi chote cha shilingi 63,800,000,” alisema Mwalimu Oregen na kuishukuru serikali kwa jitihada za kushirikiana na sekta binafsi kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu.

Alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya jitihada za kujiandaa kikamilifu kwa mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028 ili kuendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu nchini.

Akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Kituo cha Afya Magoto kilichopo kata ya Nyakonga, Mwang’onda pia alifurahishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao utagharimu shilingi zaidi ya milioni 200 hadi kukamilika kwake.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Mwang'onda (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto aliyevaa skafu) na viongozi wengine wakifurahia uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa jengo la mama na mtoto katika Kituo cha Afya Magoto.

“Mwenge wa Uhuru umefika na kukagua mradi wa jengo la mama na mtoto hapa Nyakonga na unaendelea vizuri. Wadau hawa wa Barrick wanafanya kazi kubwa na tunawashukuru sana kwa kurudisha sehemu ya faida yao katika jamii,” alisema.

Miradi hiyo ni sehemu ya miradi mipya 103 ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime chini ya mpango wa CSR Barrick North Mara.

Mwang’onda aliendelea kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta mageuzi makubwa ya uboreshaji wa sekta ya afya, ikiwemo huduma kwa wajawazito.

Alisema Rais Samia anaidhinisha utoaji wa fedha nyingi kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya afya katika halmashuri zote nchini.

“Rais anapeleka huduma za afya karibu na wananchi, hataki kuona wananchi, hasa akina mama wakisafiri umbali mrefu, anapeleka majengo ya mama na mtoto kila sehemu, lengo kubwa ni kuona wanajifungulia katika maeneo ya karibu, siyo kusafiri umbali mrefu.

“Rais Samia haishii kujenga majengo tu, anapeleka vifaa tiba vya kisasa, akina mama sasa hivi hawahangaiki, hata ukienda zahanati unakuta vifaa tiba vya kisasa, hataki kuona akina mama wakipata tabu tena,” aliongeza Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Meneja Mahusiano Msaidizi wa Barrick North Mara, Nasieku Kisambu, akipokea Mwenge wa Uhuru jana.

Mwang’onda alisema uwekezaji wa mabilioni ya fedha za CSR kutoka kampuni ya Barrick ambayo inaendesha migodi wa dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals ni ushadi wa matunda ya sera nzuri ya uwekezaji iliyopo nchini.

Aliihakikishia Barrick kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wanaoshirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo, huku akiitaka kampuni hiyo ya uchimbaji madini kuendeleza mchango wake katika sekta za kijamii.

“Endeleeni kushirikiana na serikali yetu inawapenda sana na iko tayari kuwawekea mazingira fariki ili muendelee kuchapa kazi katika taifa letu, endeleeni kufanya kazi, mko kwenye mikono salama ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, Mwang’onda aliwapongeza viongozi wa wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara kwa ushirikiano wao na sekta binafsi, akisema juhudi hizo zimekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi.

“Nishukuru viongozi kwa kazi kubwa mnayofanya kwa kushirikiana na wadau hawa wa maendeleo, endeleeni kufanya hivyo kwani serikali yetu inategemea sana sekta binafsi, lakini pia inaonesha jinsi ambavyo mnashirikiana na wananchi ili kuifanya Tarime iweze kusonga mbele kimaendeleo,” alisema Mwang’onda.
Mwang’onda alitumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa wananchi wa Tarime kuendelea kulinda amani na utulivu, akieleza kuwa mazingira ya utulivu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya jamii.

“Nawaomba sana wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu ili nchi yetu iendelee kubaki tulivu viongozi wetu wakiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan waendelee kuiletea maendeleo makubwa zaidi.

“Ndugu zangu wana-Tarime, palipo na amani ndipo penye maendeleo, ndiyo maana Mhe. Mbunge [Mwita Waitara] amesema ‘hapa ni kazi tu na maendeleo kwa sababu Tarime ina amani na utulivu’, hivyo niwaombe sana endeleeni kushikilia hapo hapo.

“Endeleeni kulinda sana amani na utulivu ili nchi yetu iendelee kusonga mbele kimaendeleo, ili Tarime yetu iendelee kusonga mbele kimaendeleo,” alisisitiza Mwang’onda.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, alisema miradi ya CSR Barrick North Mara imetapakaa katika halmashauri hiyo.

“Miradi ya CSR ipo katika kata 26, na kwenye sekta za afya, elimu, maji na barabara. CSR impenguza hata mzigo kwa wananchi kuchangia miradi,” alisema Waitara.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, alisema miradi ya CSR Barrick North Mara imeisaidia jamii
“Kwa mfano Shule ya Sekondari Matongo, asilimia Zaidi ya 90 ya majengo yake yamejengwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara. Barrick ina vitu ambavyo imejenga Matongo, ndiyo maana mahusiano yanazidi kuimarika,” alisema Ryoba.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara imetumia shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019 ulipokabidhiwa kwa Barrick.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages