Afisa Mahusiano wa Matongo Gold Mine, Adella Saitabau (wa pili kulia), akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Matongo jana Jumatatu, mara baada ya kuwakabidhi msaada wa 'rim paper' 50 za uchapishaji wa mitihani ya darasa la nne na la saba.
Tarime
-----------
Mgodi wa Dhahabu wa Matongo (Matongo Gold Mine - MGM) umetoa msaada wa ‘rim paper’ 50 za karatasi kwa ajili ya uchapishaji wa mitihani ya majaribio ya darasa la nne na la saba katika shule za msingi saba zilizopo kata ya Matongo wilayani Tarime, Mara.
Shule hizo ni Matongo, Kwihore, Nyabichune, Kenyangi, Matare, Nyamongo na Maryo, zenye wanafunzi zaidi ya 900 wa madarasa hayo.
Akikabidhi msaada huo kwa viongozi wa kata hiyo jana Jumatatu, Afisa Mahusiano wa MGM, Adella Saitabau, alisema mgodi huo umeamua kutoa mchango huo kama sehemu ya kurejesha kwa jamii faida iliyotokana na uchimbaji wa madini.
“Leo MGM tumekabidhi rim paper 50 kusaidia wanafunzi wa darasa la nne na la saba kwa ajili ya mitihani yao,” alisema Adella.
Alisema lengo ni kuchangia kuimarisha maandalizi ya wanafunzi wa madarasa hayo kuelekea mitihani ya taifa ijayo, ambapo karatasi hizo zitatumika kwenye mitihani ya majaribio ya kuwapima na kuongeza kiwango cha ufaulu.
Adella (katikati) akikabidhi msaada wa rim paper hizo kwa viongozi wa kata ya Matongo.
Adella alisema moja ya vipaumbele vya MGM ni kushirikiana na jamii inayozunguka mgodi huo katika kuboresha sekta muhimu za maendeleo, ikiwemo elimu.
Aliongeza kuwa mgodi huo unaamini kwamba maendeleo yake yanapaswa kwenda sambamba na ustawi wa wananchi kupitia uwekezaji katika huduma za kijamii.

Makabidhiano yakiendelea. (Picha zote na Mara Online News)
Kwa upande wao, viongozi wa kata ya Matongo waliushukuru Mgodi wa Dhahabu wa Matongo kwa msaada huo, wakieleza kuwa utakuwa na mchango mkubwa katika maandalizi ya mitihani ya majaribio kwa wanafunzi wa darasa la nne na la saba.
Walisema upatikanaji wa karatasi hizo utarahisisha uchapishaji wa mitihani ya majaribio kwa wakati ili kuwawezesha wanafunzi kufanya mazoezi ya kutosha kabla ya mitihani ya taifa, hivyo kuongeza matarajio ya kufanya vizuri.
“Nishukuru uongozi wa Mgodi wa Matongo kwa kutuunga mkono kwa msaada wa ream kwa wakati mwafaka. Mitihani ni muhimu kwa wanafunzi kufanya vizuri na kupata matokeo bora,” alisema Afisa Elimu Kata ya Matongo, Mwalimu Alex Simion Kayombo.
Mwalimu Kayombo aliomngeza: ‘Naamini hizi rim paper 50 zitasaidia ufanyikaji wa mitihani ya darasa la nne na la saba, maana wanafunzi hawa wanajiandaa kwa ajili ya mitihani ya kitaifa, kwa hiyo tutakuwa na maandalizi mema na matokeo bora.”
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Matongo, Jimmy Abeid, aliushukuru mgodi huo kutoa hizo karatasi na kutumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wawekezaji na wadau wengine kuiga mfano huo wa MGM.
“Kwa niaba ya kata ya Matongo, napenda kutoa shukrani za dhati kwa uongozi wa Mgodi wa Matongo kwa kutupa hizi rim paper 50. Nitoe rai kwa kampuni nyingine kuhamasika kujitokeza kuzisaidia shule zetu,” alisema Abeid.
Matongo ni moja ya migodi ya dhahabu iliyopo katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime ambalo limejaaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini aina ya dhahabu.
No comments:
Post a Comment