NEWS

Sunday, 2 August 2026

Wadau waunga mkono mkakati wa Barrick kupata wataalamu sekta ya madini Tanzania



Meneja Ugavi wa Barrick North Mara, Enock Otieno, akizungumza katika mdahalo wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Tano la Utekelezaji na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini uliofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.

Na Mwandshi Wetu
---------------------------

Mkutano wa Jukwaa la Tano la Utekelezaji na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini uliofanyika Mwanza hivi karibuni ulitoa maazimio mbalimbali, likiwemo la kuwekeza kwenye rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Tayari kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick yenye ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals imeanza kuchochea ukuaji wa sekta hiyo kwa kuwezesha taifa kupata wataalamu wa madini na jiolojia.

Kwa kutambua kuwa tasnia ya madini inajumuisha mambo mengi zaidi ya uchimbaji, Barrick kuanzia mwaka jana imeanza kufanya kazi na taasisi za elimu ya juu na kati kwa ajili ya kusuka kizazi kijacho cha wataalamu wa madini wazawa, ambapo imefadhili wanafunzi watano Watanzania kusoma taaluma ya madini nje ya nchi.

Barrick imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo itatoa shilingi bilioni 26 ili kuleta tija na ufanisi katika kukuza sekta ya madini kwa kuongeza tafiti, nguvu kazi ya wataalamu, ubunifu na kuwajengea uwezo wanafunzi wanaosoma fani ya madini kuanzia ngazi ya shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na uzamivu.

Pia, Barrick ina programu ya wataalamu wabobezi kutoka kwenye kampuni ili kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma taaluma ya madini kwenye vyuo vikuu, ambapo mapema mwaka huu, yaliwafikia wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Shule ya Madini na Jiolojia (SoMG) ya Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha, Barrick imekuwa inatoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati wanaosoma fani mbalimbali kufanya mafunzo ya vitendo katika migodi yake ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu.

Akitoa mada ya uzalishaji wa rasilimali watu unaoendana na ukuaji wa teknolojia mpya katika sekta ya madini nchini, Mkuu wa Kitivo cha Shule ya Madini na Sayansi ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Elisante Mshiu, alisema kwa sasa uwekezaji mkubwa unaendelea kwenye sekta ya madini na mabadiliko ya teknolojia.

Sehemu ya washiriki wa mkutano wa jukwaa hilo

Hivyo, Prof. Mshiu alisema wadau wote waliopo katika tasnia ya madini wanapaswa kuungana na kutambua kuwa biashara ya madini si kuchimba pekee, bali kunahitajika kuwekeza kupata rasilimali watu ya kizazi kipya yenye ujuzi wa kisasa, ambayo itaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya Akili Unde (AI).

Alisema wakati kasi ya wawekezaji katika tasnia inakua na uwepo wa sheria za kuwezesha wazawa kunufaika na mnyororo wa sekta ya madini, suala la kuwekeza kwenye elimu haliepukiki kwa ajili ya kupata nguvu kazi yenye utaalamu kuanzia kwenye masuala ya jiolojia, uhandisi wa madini, uchenjuaji, biashara na sheria, mifumo ya TEHAMA, ugavi, usafirishaji na taaluma nyingine zinazohusu mnyororo mzima wa kufanya kazi na biashara kwenye migodi.

Prof. Mshiu alitoa ushauri kwa kampuni zote zinazohusiana na madini na wadau wote kulipa kipaumbele suala la kushirikiana na taasisi za elimu ya juu kujenga kizazi cha wataalamu katika tasnia na kuwa tayari kutoa nafasi za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.

Alisema hatua hiyo itawawezesha wahitimu masomo hayo kuwa na ujuzi wa kutosha unaohitajika katika soko kuendana na shughuli mbalimbali katika mnyoyoro mzima wa tasnia ya madini kama ambayo kampuni ya Barrick imeanza kuonesha njia.

Naye Kamishna Msaidizi wa Tume ya Madini kutoka nchini Ghana, Victoria Awuni, ambaye alikuwa mmoja wa watoa mada kutoka nje ya nchi katika mkutano huo, alisema ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini haumaanishi kuuza huduma na bidhaa migodini tu, bali kunahitajika uwekezaji wa dhati wa wadau katika kupata wataalamu wazawa wenye ujuzi wa kuendesha migodi na shughuli nyinginezo zinazohusiana na tasnia hiyo.

Alieleza kuwa njia ya kuwapata wataalamu hao ni pamoja na kushirikiana kwa karibu na vyuo vya elimu, sambamba na kutoa nafasi za kutosha kwa wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo kwenye migodi na kampuni zinazohusika na shughuli za migodini.

Awuni alisema Serikali ya Ghana kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya madini imekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika elimu ili kupata wataalamu wa kutosha, ambapo nchi hiyo imefanikiwa kwa kuwa na wataalamu wengi wanaofanya kazi katika migodi mbalimbali nje ya nchi.

Kwa upande wake Mhadhiri kutoka Shule ya Madini ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Morris Hijji, akizungumza katika mdahalo wa ukuzaji sekta ya madini nchini, alitoa wito kwa wadau kufanya kazi kwa karibu na taasisi za elimu ya juu ili ziweze kuandaa wataalamu wanaokidhi viwango vinavyotakiwa katika soko, sambamba na kutoa nafasi za kutosha kwa wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo kulika nadharia.

“Chuo Kikuu cha UDOM tumejipanga kufanya kazi kwa karibu na wadau katika tasnia ambao watakuwa tayari kutoa ufadhili wa wanafunzi, tafiti na nafasi za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi, lengo kubwa likiwa ni kufanikisha kupata wataalamu wenye ujuzi unaohitajika kwendana na mabadiliko ya teknolojia ya uendeshaji muima wa mnyororo wa sekta ya madini nchini na sheria ya ushirikishwaji Watanzania katika tasnia ya madini,” alisema Dkt.H ijji.

Naye Mkuu wa Masuala ya Ugavi kutoka Benki ya Absa nchini Afrika Kusini, akitoa mada kuhusiana na huduma za ugavi wa kitaalamu na kisasa, alisema katika zama tulizonazo kunahitajika wataalamu wenye utaalamu wa kutosha katika kufanya kazi na kampuni kubwa ikiwemo migodi, wanaoelewa mifumo mbalimbali ya biashara, sheria, teknolojia na jinsi ya kufanya kazi na wadau wa nje inapobidi.

Alitoa ushauri kwa wadau wote waliopo kwenye tasnia ya madini kuwekeza kwenye elimu kwa lengo la kupata wataalamu wa fani mbalimbali ili taifa liwe na wataalamu wa kutosha, wakiwemo wanaoelewa programu zinazotumika katika shughuli za utafiti, uchimbaji na nyingine zinazohusiana na madini.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa jukwaa hilo, Waziri wa Madini, Antony Mavunde, alisema kuna ongezeko la uwekezaji katika sekta ya madini na kwamba matarajio ya kuanzishwa kwa migodi mipya yafungua fursa zaidi kwa Watanzania kupata ajira.

Waziri Mavunde akizungumza katika mkutano huo

Hivyo, Waziri Mavunde alitoa wito kwa watoa huduma kujiandaa kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani, kuongeza ubora wa bidhaa, huduma na kujenga uwezo wa kushindana katika soko, huku akigusia kuwa migodi mingine mipya 13 inakwenda kufunguliwa nchini.

Alisema serikali imeendelea kushuhudia ongezeko la ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa kwenye migodi tangu kufanyika kwa maboresho ya Sheria ya Madini, Sera na Kanuni zake za mwaka 2009, ambao unakwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Aidha, pamoja na mambo mengine, aliwataka watoa huduma katika migodi nchini kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja ili kuchangamkia fursa zinazoongezeka katika sekta hiyo, hususani katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma bora zinazokidhi viwango vinavyohitajika kwa wawekezaji kwenye sekta ya madini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages