
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, Agosti 10, 2026.
---------------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo maalum na Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini, kupitia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Mazungumzo hayo yalifanyika Agosti 10, 2026 Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ikulu baadaye siku hiyo, ilisema walijadili masuala mbalimbali ya kitaifa yanayogusia jamii, yakiwemo ya kisiasa, imani na maendeleo, pamoja na kuimarisha amani, mshikamano na kujenga mustakabali mwema wa taifa.
Pia, mazungumzo hayo yaligusia umuhimu wa nafasi ya madhehebu na viongozi wa dini katika kulea jamii yenye maadili mema, uwajibikaji na mshikamano, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika ustawi na maendeleo endelevu ya taifa.
Rais Samia aliwashukuru Maaskofu hao kwa kuona umuhimu wa kukutana na kujadiliana naye masuala yenye tija kwa taifa.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwahakikishia viongozi hao wa kiroho dhamira yake ya kuendeleza utamaduni wa kushauriana na kushirikiana na viongozi wa dini na makundi mbalimbali katika jamii kuhusu masuala muhimu ya kitaifa kila inapohitajika.
No comments:
Post a Comment