NEWS

Friday, 25 September 2026

Serikali yabadili ratiba ya mitihani ya taifa kukwepa athari za El Nino




Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
----------------------

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imerekebisha ratiba ya upimaji na mitihani ya taifa kwa mwaka 2026 kwa lengo la kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwezekano wa mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Wanu Hafidh Ameir (katikati pichani juu), amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya serikali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na kutathmini athari zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa upimaji na mitihani ya taifa.

Wanu amesema kwa mujibu wa utabiri rasmi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuna uwezekano wa kutokea kwa El Nino yenye nguvu, inayotarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo nchini Oktoba na kuwa nyingi zaidi Novemba 2026, hali inayoweza kuathiri usafiri na kufikika kwa baadhi ya vituo vya mitihani.

Ameeleza kuwa kwa kuzingatia jiografia ya nchi na uwezekano wa baadhi ya maeneo kukumbwa na mafuriko, changamoto za usafiri na athari nyingine zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya taifa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyorekebishwa, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili Ngazi ya Shule utafanyika Oktoba 7 hadi 8, 2026, wakati Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 hadi 6, 2026.

Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili utafanyika Oktoba 12 hadi 23, 2026 na Mitihani ya Kidato cha Nne itafanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026.

Naibu Waziri Wanu amesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi, maafisa na wadau wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, lakini pia kulinda mitihani, vifaa na nyaraka muhimu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages