
Na Mwandishi Wetu
Lango jipya la Lemiyoni limefunguliwa katika wilaya ya Monduli mkoani Arusha, ili kuboresha shughuli za utalii na uwekezaji.
Uzinduzi wa lango hilo litakalounganisha Hifadhi ya Taifa Tarangire na Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Landilen (WMA), ulifanywa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Kimath.
Lengo linatarajiwa kurahisisha shughuli za utalii, ambapo watalii kutoka Landilen WMA wataingia Hifadhi ya Tarangire kwa urahisi zaidi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), mradi wa ujenzi wa lango hilo umegharimu shilingi milioni 76.7.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo uliohudhuriwa na wananchi waliokuwa wakicheza ngoma za jadi, Mkuu wa Wilaya, Kimath, aliwashukuru wadau wa maendeleo walioshiriki kwa hali mali kuhakikisha kuwa ujenzi wa lango hilo unakamilika kama ilivyokusudiwa.
Wadau hao ni pamoja viongozi wa TANAPA, Hifadhi za Tarangire na Landilen WMA, Honeyguide Foundation, wawekezaji na waendeshaji wa utalii na wananchi wanaoishi kuzunguzuka hifadhi zote mbili katika wilaya za Babati na Monduli ambao wamekuwa chachu ya kukuza shughuli za utalii.
Lango la Lemiyoni ni matokeo ya juhudi za miaka minane tangu wazo la kuanzishwa kwake libuniwe mwaka 2018, kwa mujibu wa maelezo ya Kimath.
Eneo la kaskazini mwa Tanzania linasifika kwa shughuli za utalii kwa kuwepo vivutio vya utalii, hasa Hifadhi za Taifa na Mlima Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment