
Sehemu ya mabasi ya abiria yakiwa yameegeshwa katika kituo cha Tarime baada ya madereva husika kugoma kuingia kazini leo asubuhi Jumanne, Septemba 29, 2026.
Tarime
-------------
Madereva wa mabasi na magari mengine ya abiria katika kituo cha Tarime mkoani Mara, wamegoma kuingia kazini wakilalamikia mfumo mpya wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani (Trafiki) wa kukata alama kwenye leseni zao wanapofanya makosa ya barabarani.
Wamedai kuwa hatua hiyo ya Jeshi la Polisi ni kandamizi na kwamba baadhi ya adhabu za makosa wanayokutwa nayo kazini zinastahili kuelekezwa kwa wamiliki au waajiri wao.
Mara Online News imefika katika kituo cha mjini Tarime na kushuhudia mgomo huo ukiendelea kuanza asubuhi leo Jumanne, Septemba 29, 2026 huku mabasi yaendayo mikoani na maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wa Mara yakiwa yameegeshwa ndani ya kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya, Mark Njera, amefika kituoni hapo kwa ajili ya kuzungumza na madereva pamoja na wamiliki wa magari husika ili kutafuta suluhu ya mgomo huo.
Mgomo wa maderava wa magari ya abiria umeripotiwa kuanza leo asubuhi pia katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Dar es Salama, Mwanza, Kahama, Serengeti, Sirari na Nyamongo.
Mgomo huo umesababisha abiria waliokuwa wamepanga kusafiri kwenda maeneo mbalimbali kukwama katika kituo hicho.
Abiria waliokwama katika kituo cha Tarime ni ambao walipanga kusafiri leo kwenda maeneo mbambali nchini, ikiwemo Dar es Salama, Mwanza, Kahama, Dodoma, Musoma, Serengeti, Nyamongo, Sirari na Shirati.

Chini ya utaratibu huo wa Jeshi la Polisi unaotokana na Tangazo la Serikali Na. 420 (G.M. No. 420), kila leseni ya udereva ina pointi 15 zinazopunguzwa kulingana na uzito wa kosa linalofanywa na dereva.
Madereva hao wanapinga utaratibu huo wakidai baadhi ya makosa, yakiwemo kutumia tairi mbovu au kuendesha gari lenye hitilafu, yanastahili kuelekezwa kwa mwajiri au mmiliki wa gari badala ya dereva kukatwa alama kwenye leseni yake.
Hivyo, wameeleza hofu yao ya kupoteza alama hizo na hatimaye kufungiwa leseni, hali inayoweza kuwakosesha sifa za kuendelea na udereva na hivyo kuyumba kimaisha.
Mwenyekiti wa Umoja wa Maderev awa Mabasi Tanzania (UWAMATA), Majura Kafumu, amethibitisha kutokea kwa mgomo wa madereva wa mabasi katika maeneo mbalimbali nchini.
Madereva hao na abiria waliokwama wameomba serikali na mamlaka husika kuingilia kati suala hilo, ikiwemo kuwakutanisha wadau ili kujadili utekelezaji wa mfumo huo wa Jeshi la Polisi.
Aidha, wameomba serikali kuchukua hatua haraka za kuhakikisha huduma za usafiri zinarejea ili kuwaondolea wananchi usumbufu.

Sehemu nyingine ya magari ya abiria yakiwa yameegeshwa katika kituo cha Tarime. (Picha zote na Mara Online News)
Septemba 19, 2026 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alisema mfumo wa alama za leseni za udereva bado haujaanza kutekelezwa rasmi na kuwataka madereva kutokuwa na wasiwasi kuhusu kupunguzwa kwa alama kwenye leseni zao.
Waziri Katambi alisema kinachoendelea kwa sasa ni majaribio ya utekelezaji wa Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, zilizorekebishwa mwaka 2025, sambamba na utoaji wa elimu kwa umma.
Alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa kuna umuhimu wa kuwepo mfumo wa kudhibiti makosa ya usalama barabarani yanayochangiwa na madereva.
Aliongeza kuwa mamlaka ya kutunga kanuni hizo inatokana na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, inayompa waziri uwezo wa kuweka taratibu za kuimarisha usalama wa watumiani wa barabara.
Katambi alisema mfumo huo ni mkakati wa serikali wa kupunguza ajali za barabarani, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kamera za kisasa zinazotumia akili unde (AI) katika baadhi ya barabara kuu.
No comments:
Post a Comment