NEWS

Monday, 14 September 2026

Programu ya Madini kwa Kesho Njema, injini ya kuwainua wachimbaji wadogo nchini



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa programu ya Madini kwa Kesho Njema (Mining for aBrighter Tomorrow - MBT) akiwa na viongozi wa vyama vya madini na wawakilishi wa wachimbaji wadogo katika viwanja Ingwe, Nyamongo wilayani Tarime, hivi karibuni.

Na Damas Makangale
Aliyekuwa Tarime
--------------------------

Kupitia Sheria ya Madini ya Mwaka 1998, Tanzania ilianzisha leseni ndogo za uchimbaji wa madini nchini (Primary Mining License), ikiwa ni moja ya hatua muhimu katika kuwafungulia milango Watanzania kushiriki katika shughuli za uchimbaji mdogo.

Kuanza utekelezaji wa sheria hiyo kuliwezesha wachimbaji wadogo kumiliki leseni na safari ya urasimishaji ilipoanza na ushiriki wa Watanzania katika sekta uliongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa takwimu, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa watu zaidi ya milioni sita wanajihusisha na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani madini.

Akitoa risala kwenye uzinduzi wa programu ya Madini kwa Kesho Njema (Mining for a Brighter Tomorrow) na helikopta ya utafiti wa madini ya Kampuni ya Barrick hivi karibuni Nyamongo wilayani Tarime, Kamishna Msaidizi na Msimamizi wa programu hiyo, Mhandisi Amini Msuya, alisema kati ya watu milioni sita, asilimia 51.3 ni wanawake, asilimia 67.8 wana umri kati ya miaka 18-45 na watu zaidi ya laki mbili ambayo ni sawa na asilimia 3.82 walikuwa wenye ulemavu.

Mhandisi Msuya alisema programu hiyo ni hatua muhimu katika jitihada za serikali za kuhakikisha kuwa ukuaji wa sekta ya madini unaenda sambamba na ushiriki mpana, usawa na manufaa kwa wananchi, hususan vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum.

“Takwimu hizi zinaonesha kuwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum si kundi dogo katika sekta ya madini, bali ni sehemu muhimu ya nguvu kazi katika sekta.

Hata hivyo, pamoja na uwepo wao, bado ushiriki wao haujafikia kiwango kinacholingana na uwezo na fursa zilizopo. Hapo ndipo chimbuko la programu ya MBT lilipoibuliwa ili kuhakisiha ushiriki wa kundi hili unaongezeka kwa kasi nchini nzima.

“Nchi yetu imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini, hususan mabadiliko katika Sera na Sheria ya Madini.

“Mabadiliko hayo yameweka mazingira ya kukuza uwekezaji, kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini ,” alisema Mhandisi Msuya.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikiendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha ushiriki wa kundi hili muhimu unaongezeka na kunufaika na rasilimali madini yaliyopo hapa nchini, mathalani sera ya madini ya mwaka 2009 imeelekeza serikali kuchukua hatua za kuwezesha Watanzania kushiriki na kunufaika katika mnyororo wa thamani madini, huku ikihamasisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini nchini.

“Katika kutekeleza azma hiyo, serikali imechukua hatua mbalimbali, zikiwemo kufanya maboresho ya sheria na mifumo ya usimamizi; urasimishaji wa wachimbaji wadogo ikihusisha kuwapa leseni na kusimamia ipasavyo shughuli zao za uchimbaji na uchenjuaji; kuanzishaji vituo vya ununuzi na masoko ya madini; kuanzishwa kwa vyama vya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini; na kutoa huduma za jiosayansi,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, programu hiyo itatekelezwa kwa muda wa miaka mitano 2025-2030 kwa kushirikiana kati ya Wizara ya Madini, wadau na washirika mbalimbali na inalenga ushiriki zaidi wa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum ili kuongeza tija na manufaa yatokanayo na sekta ya madini.

“Ni programu yenye kusudio la moja kwa moja la kuongeza ajira kwa makundi hayo sambamba na kufunganisha sekta ya madini na zingine ili kuendelea kukuza mnyororo wa thamani nchini, na kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa mitaji, vifaa na teknolojia,” aliongeza Mhandisi Msuya.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo, alisema programu ya MBT ni shauku na matamanio ya serikali katika kuwasaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuingia rasmi na kushiriki zaidi kwenye sekta ya madini.

Aliongeza kwamba serikali kupitia Taasisi za Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imepima ramani ya madini kwa asilimia 97 na utafiti wa kina na mipasuko wa miamba kwa asilimia 16 tu.

“Kutokana na taarifa hizo, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassa alitoa maelekezo ya kutenga asilimia 10 ya mapato yanayotoka kwenye sekta ya madini ili kufanya utafiti wa kina nchini nzima.

Waziri Mavunde alisema serikali imefikia hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya madini baada ya kuridhia kutenga asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na sekta hiyo kwa ajili ya kugharamia utafiti wa kina wa rasilimali za madini nchini.

“Natoa maelekezo na maagizo hapa kwamba kila Afisa Madini wa Mkoa nchini nzima kuanza mchakato wa mara moja wa kutenga maeneo ya wachimbaji wadogo na ikitokea nimekuja mwenyewe kwenye mkoa wako na hujatenga maeneo nifuate nyuma,” alisema Waziri Mavunde.

Waziri Mavunde akizindua helikopta ya kisasa ya Kampuni ya Barrick kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga wenye kupunguza athari za kimazingira, kuongeza kasi ya utafiti wa kisayansi na kuboresha shughuli za utafutaji wa madini, kufanikisha utekelezaji wa program ya MBT inayolenga kuwezesha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa helikopta hiyo sambamba na programu hiyo uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe Nyamongo wilayani Tarime, Waziri Mavunde aliongeza kuwa mahusiano kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na wachimbaji wadogo na wananchi wa Nyamongo unazidi kuimarika kwa pande zote kuanza kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi mapana ya taifa.

Aliongeza kwamba mpango wa Kampuni ya Barrick kuongeza nyenzo za kufanya utafiti wa kijiolojia kwenye eneo lao la kilomita za mraba 6,000 na kwa mita 30 kutoka ardhini kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu ya kisasa zaidi (high-resolution airborne geophysical surveys) ambayo huongeza usahihi wa upatikanaji wa taarifa za miamba iliyo chini ya ardhi, kupunguza athari za kimazingira, kuongeza chachu ya utafiti wa kisayansi, kitaalamu na kuboresha ufanisi wa shughuli hizo.

“Baada ya mashauriano na uongozi wa Barrick kuhusu namna ya kufanya kazi na wananchi wa maeneo haya, Barrick walikubali kurudisha leseni ya baadhi ya maeneo ambayo ilifanya tafiti zikagawiwa kwa vijana wa Nyamongo kwa ajili ya uchimbaji mdogo mdogo.

“Lakini leo hii tunaanza safari ya mafanikio makubwa na vijana wa Nyamongo wanaanza uchimbaji wa madini kwa uhakika zaidi baada ya kampuni ya Barrick kukubali kutoa helikopta yake kwa ajili ya utafiti wa kitalaamu kwenye maeneo yao, haya ni mafanikio makubwa kwa vijana, akina mama na watu wenye mahitaji maalum kwenye wilaya ya Tarime,” alisisitiza Waziri Mavunde.

Vilevile, Waziri Mavunde akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma hivi karibuni, alisema hatua hiyo ya kutaka kufanya utafiti wa kina ni ya kihistoria na itawezesha Tanzania kuongeza uelewa wa kina kuhusu utajiri wa madini uliopo katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema Tanzania imepiga hatua katika shughuli za utafiti wa jiolojia ambapo hadi sasa imefanya ‘geological mapping’ kwa asilimia 97, ‘geochemical survey’ kwa asilimia 24 na ‘low resolution survey’ kwa asilimia 100 tangu tafiti hizo zilipoanza kufanyika miaka ya 1978 na 1979.

Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini nchini na kufungua milango ya tafiti kwa kutumia nyenzo za kisasa na kuwashirikisha wachimbaji wadogo ili kupanua mnyororo wa thamani wenye kutoa matokeo chanya kwa wawekezaji na Watanzania kwa ujumla.

Dkt. Ngido aliongeza kuwa uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ni muhimu katika utekelezaji wa Sera ya Madini ya Taifa, inayolenga kuimarisha utafiti wa rasilimali madini, kuongeza thamani ya sekta ya madini katika uchumi wa taifa na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa ufanisi zaidi, huku uchangiaji kwenye maendeleo ya nchi ukiendelea kukua kwa kasi na kugusa sekta zote mtambuka.

“Napenda kuchukua fursa hii kukushuru Waziri wa Madini, Mavunde, kwa kila jambo ambalo umekuwa ukiahidi unalitekeleza kwa ufanisi mkubwa ili kuweza kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye mapato, ajira na ukuzaji wa mnyororo wa thamani,” alisisitiza Dkt. Ngido.

Alifafanua kuwa wameshiriki katika utekelezaji wa programu hiyo, ikiwa ni pamoja na kurudisha serikalini sehemu ya leseni zake za utafiti wa madini kwa ajili ya kunufaisha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum katika kuunga mkono juhudi za serikali za kutaka kuleta mapinduzi ya kijani kwa sekta ya madini nchini.

"Sisi kama North Mara (Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara) tumerudisha leseni za utafiti 50 kwa vijana karibia 2,000 ambazo watapanua wigo wa uchimbaji na utafutaji wa madini," alisema Dkt. Ngido.

Migodi ya dhahabu ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ambao upo kwenye hatua za ufungaji wilayani Kahama, Shinyanga, inaendeshwa kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages