
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wilayani Itilima, Simiyu jana Jumatatu.
Itilima
------------
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Waziri wa Kilimo kukutana na wadau wa pamba na ndani ya siku 30 kuwasilisha mapendekezo ya mfumo bora wa ununuzi wa pamba utakaonufaisha wakulima na kuendeleza uzalishaji wa zao hilo.
Dkt. Mwigulu alitoa agizo hilo Septemba 14, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, baada ya Mbunge wa jimbo la Itilima, Njalu Daudi Silanga, kueleza changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba, ikiwemo malalamiko kuhusu mfumo wa sasa wa ununuzi.
“Leo tarehe 14, mpaka tunapofika tarehe 14 mwezi ujao, niwe nimeshapata taarifa ya utaratibu mzuri ambao tutakubaliana,” aliagiza Waziri Mkuu Mwigulu.
Alisema serikali italinganisha mifumo iliyowahi kutumika na unaotumika sasa ili kupata utaratibu utakaokuwa na manufaa zaidi kwa wakulima bila kuathiri uzalishaji, bei ya pamba na maisha ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu alisema serikali imeondoa sheria iliyokuwa ikiruhusu mifugo ya wananchi kutaifishwa na kuelekeza mapitio ya sheria na kanuni nyingine zinazohusiana na mifugo.
Pia, alielekeza kulipwa kwa wananchi ambao mifugo yao ilitaifishwa na baadaye wakashinda kesi mahakamani.
Waziri Mkuu huyo pia alisisitiza kuwa vyombo vya serikali havipaswi kuchukua bodaboda, bajaji, baiskeli, mikokoteni au mali nyingine zinazotumiwa na wananchi kujipatia kipato kwa ajili ya kukusanya faini, bali faini zitolewe kwa mujibu wa sheria bila kumnyang’anya mwananchi chombo chake cha kazi.
Kuhusu bei ya saruji, Dkt. Mwigulu alisema serikali imeanza kuchukua hatua baada ya kubaini bei kufikia hadi shilingi 27,000, 30,000 na 32,000 katika baadhi ya maeneo.
Waziri Mkuu Mwigulu aliwaagiza wataalamu husika kuandaa mpango wa kimkakati wa kurekebisha hali hiyo ndani ya wiki moja.
Aidha, alisisitiza kuwa mgonjwa anayehitaji rufaa hapaswi kuombwa fedha ya mafuta ya gari la wagonjwa. “Kuanzia sasa, mgonjwa asiombwe fedha ya kujaza mafuta kwenye gari la wagonjwa,” alisema.
Dkt. Mwigulu alisema serikali imeelekeza shilingi zaidi ya trilioni 1.4 mkoani Simiyu katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umeme, barabara, maji, elimu na afya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, alisema serikali inaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na mwingiliano kati ya shughuli za wananchi na wanyamapori, waikiwemo wananchi walioathiriwa na wanyamapori na wanaostahili kulipwa fidia.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Festo John Dugange, alisema katika siku 100 za mwanzo za Serikali ya Awamu ya Sita, wilaya ya Itilima ilipata watumishi 51 wa afya na walimu 135.
Mbunge wa Itilima, Njalu Daudi Silanga, alisema wilaya hiyo imeendelea kupata uwekezaji katika sekta za elimu, afya, maji, barabara na umeme, huku akiwasilisha changamoto zinazoendelea kuhitaji hatua za serikali.
No comments:
Post a Comment