NEWS

Sunday, 15 November 2026

Madiwani Serengeti watoa tamko uharibifu wa mazingira Bwawa la Manchira



Sehemu ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti wakiendelea na kikao chao kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo Novemba 13, 2026.

Na Joseph Maunya
Serengeti
----------------

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wametaka jitihada ziongezwe kudhibiti uharibifu wa mazingira yanayozunguka chanzo cha maji cha Bwawa la Manchira.

Walitoa azimio hilo Novemba 13, 2026 wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, ambapo suala la uharibifu wa chanzo hicho cha maji liliibua mjadala mkubwa.

Baadhi ya madiwani walisema kuna watu wanadaiwa kulisha mifugo yao katika bwawa hilo na kuchangia uharibifu wa mazingira yanayozunguka chanzo hicho muhimu cha maji.

"Kuna baadhi ya watu, tena wengine wana nguvu kubwa ya kifedha wanapeleka mifugo yao kuchunga katika eneo la bwawa, hali inayoharibu mazingira ya pale na kuliweka hatarini bwawa lile," alisema Diwani wa Kata ya Uwanja wa Ndege, Matoke Joseph Michael maafufu kwa jina la Mapancha.

Naye Diwani wa Kata ya Manchira, Peter Elibariki Masule, alisema: "Lazima tuwawajibishe hawa watu wanaopeleka mifugo pale kuliko kubadili bodi za usimamizi wa bwawa, ili tukiokoe chanzo hiki cha maji kiendelee kutufaa sasa na hata vizazi vijavyo."

Aidha, madiwani wengi walinyoosha vidole kwa baadhi ya watumishi ambao wanafanya uzembe na kuruhusu uharibifu wa chanzo hicho cha maji ambacho ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa mji wa Serengeti na vijiji jirani.

"Sisi kama Baraza la Madiwani tunaendelea kusema hatuko tayari kuvumilia watumishi wazembe wanaosimamia mradi wa Bwawa la Manchira. Yeyote atakayethibitika kushiriki huo uharibifu achukuliwe hatua za haraka," alisema Diwani wa Kata ya Ikoma, Ezekiel Kiniba Mazanza.

Baraza hilo la madiwani lilihitimisha mjadala huo kwa kuazimia kuimarishwa kwa ulinzi wa bwawa hilo, ikiwa ni pamoja na kushirikisha vyomba vya dola na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti.

"Tunaweka azimio kwamba kile chanzo cha maji kiokolewe," alisisitiza Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na Diwani wa Kata ya Rung'abure, Elias Merengo Mwita.

Sehemu ya Bwawa la Manchira ambalo ukarabati wake umegharimu mamilioni ya fedha kutoka serikalini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages