
Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Stanslaus Mabula (aliyenyoosha mkono), akiwa kwenye ziara ya kukagua huduma katika Kituo cha Afya Utegi jana.
Rorya
------------
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Stanslaus Mabula, amehimiza watumishi wa afya kuhakikisha wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanapata huduma bila malipo kama ilivyoainishwa kwenye miongozo ya serikali.
DC Mabula alisisitiza hayo jana wakati wa ziara yake katika Kituo cha Afya Utegi alipokwenda kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kujua changamoto zinazokikabili kituo hicho.

Huku akiwa ameambatana na Diwani wa Kata ya Koryo, Daniel Akondo Omolo, DC Mabula alielezwa kuwepo upungufu wa watumishi wa afya, ukosefu wa uzio na nyumba za watumishi katika kituo hicho.
Alisema serikali imejidhatiti kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuendelea kuboresha miundombinu na kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ubora na weledi.
Hivyo, Mkuu huyo wa wilaya aliahidi kwenda kuwasilina na mamlaka za juu serikalini ili kuweka msukumo wa utatuzi wa changamoto za kituo hicho kwa kuzingatia vipaumbele.

Aidha, DC Mabula alikipongeza Kituo cha Afya Utegi kwa kuimarisha usafi wa mazingira, na akasisitiza muendelezo wa upandaji miti ili kuhifadhi mazingira katika jamii.
Vilevile, aliwapongeza madaktari na watumishi wa kituo hicho kwa kazi wanazoifanya, huku akiwahimiza kuendelea kuwahudumia wananchi kwa upendo, kuzingatia maadili ya taaluma zao na miongozo ya serikali.
No comments:
Post a Comment