
Mbunge Mwita Waitara akiwasilisha hoja bungeni
Dodoma
---------------
---------------
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara, Mwita Waitara, ameibana serikali kuhusu upelekaji wa vifaa tiba kwenye vituo vya afya vilivyokamilika katika jimbo hilo.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya afya unapaswa kwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa tiba ili wananchi waweze kunufaika na huduma zilizokusudiwa.
Katika swali lake bungeni jijini Dodoma jana Jumanne, Novemba 3, 2026, Waitara alitaka kujua ni lini serikali itapeleka vifaa tiba kwenye vituo vya afya vya Mtana, Bumera, Magoma na Kwihancha.
Alisema majengo ya vituo hivyo yamekamilishwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassa, lakini hayana huduma stahiki kwa wananchi kutokana na ukosefu wa vifaa tiba.
“Naomba nijue ni lini serikali itapeleka vifaa ili wananchi badala ya kutazama majengo mazuri yaliyojengwa na Mama Samia wapate huduma sahihi,” aliuliza Waitara.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Nnchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alisema serikali inaendelea na hatua za kuhakikisha vituo hivyo vinapata wataalamu na vifaa tiba.
Alimhakikishia Mbunge Waitara kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, Wizara za Fedha na Afya kuhakikisha vifaa tiba vinafikishwa katika vituo husika kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
“Fedha nyingi zimekwenda kujenga miundombinu katika majimbo yetu, sasa hatua inayofuatia ni kupeleka wataalamu na vifaa tiba ili vituo vya afya vitoe huduma ambazo Rais Samia anataka kuacha tabasamu kwa wananchi,” alisema Dkt. Dugange.
No comments:
Post a Comment