NEWS

Sunday, 21 July 2024

Maswi, Ridhiwan wang’ara teuzi za Rais Samia, Nape na Makamba wavuliwa uwaziri, Mashinji na Afraha wahamishwa Serengeti


Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
-------------------------------------------

Na Mara Online News
------------------------------

Eliakim Chacha Maswi ni miongoni mwa viongozi kadhaa waliong’ara katika teuzi zlizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, jana Julai 21, 2024.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt Moses Kusiluka kuhusu teuzi hizo, Maswi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.

Kabla ya uteuzi huo, Maswi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Eliakim Chacha Maswi
-------------------------------

Wakati huo huo, Rais Samia ametengua uteuzi wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye na kumteua Jerry William Silaa kuchukua nafasi hiyo.

Rais pia ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Yusuf Makamba na kumteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge na kuchukua nafasi hiyo.

Ridhiwan Jakaya Kikwete yeye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Katika hatua nyingine, Kemirembe Rose Lwota amehamishwa kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara akitokea Wilaya ya Manyoni mkoani Singida. Anachukua nafasi ya Dkt Vincent Mashinji ambaye amehamishiwa Manyoni.

Naye Maulid Suleiman Madeni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuchukua nafasi ya Afraha Nassoro Hassan aliyehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga.
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages